RAIS WA VIETNAM AMEFANYA MAZUNGUMZO NA RAIS MSTAAFU JAKAYA KIKWETE


Na Beatrice Lyimo-Dar es salaam.
 
Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na  Rais mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya  Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete leo amekutana na kufanya mazungumzo na  Rais wa Jamhuri ya  Kisoshalisti ya Vietnam Mhe. Truong Tan Sang katika ofisi ndogo za Makao makuu ya Chama cha Mapinduzi mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya mapokezi  ya Rais huyo, Dkt. Kikwete amesema kuwa lengo la ujio wa Rais wa wa Vietnam katika ofisi za CCM ni kudumisha  na kuendeleza uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya  Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Komunisti cha Vietnam.

Amesema Chama cha cha Komunisti cha Vietnam na chama cha TANU na ASP  vimekuwa  na mahusiano ya  muda mrefu  ya kihistoria toka  kipindi  ambacho vietnam ilikua ikipambana na ubeberu  wa kimarekani.

Ameeleza kuwa katika  mapambano hayo Chama cha TANU  kiliunga mkono juhudi hizo kwa kuwaunga mkono wananchi wa Vietnam katika ukusanyaji wa michango mbalimbali iliyowezesha mapambano dhidi ya Ubeberu wa Kimarekani.

Aidha, amebainisha kuwa ujio wa Rais huyo wa Vietnam kama kiongozi wa Mkuu wa Chama na Serikali katika  ofisi ndogo za Makao makuu ya CCM ni ishara ya kudumisha uhusiano mzuri uliopo baina ya vyama hivyo viwili ambavyo viko  madarakani.

Post a Comment

0 Comments