Meneja wa Shamba
Matayarisho ya kuapnda mazao mapya yakiendelea.
Mkulima akisafisha shamba kama alivyokutwa na mpigapicha wetu.
NA
KHADIJA KALILI, ALIYEKUWA CHINA
HOJA kwamba
kilimo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, imebaki katika mizania ya
nadharia zaidi kuliko vitendo.
Japo imekuwapo
misamiati mingi yenye kuvutia inayotolewa na serikali kuonyesha inavyojali
sekta ya kilimo kama ‘Kilimo Kwanza’ na mingineyo, ni ukweli wa mambo yote hayo
yamebaki katika makabrasha tu.
Ukweli wa
haya yanathibitishwa na namna serikali ilivyoshindwa kujali kwa vitendo sekta
ya kilimo ndio maana leo hii soko la mazao mengi kama kahawa, pamba, korosho,
imekuwa haina uhakika huku wakulima wanaothubutu kulima, huishia kukopwa.
Anayebisha
haya, kaulize mfumo wa stakabadhi ghalani unavyowatesa wakulima katika maeneo
mbalimbali ya nchi huku wajanja wakinufaika kwa kujenga ‘mahekalu’ ya kifahari
kwa fedha za wakulima waliobaki katika dhiki.
Kitendo cha
nchi kushindwa kuwekeza katika kilimo ambacho kingeweza kusaidia ukuaji wa
uchumi kupitia uuzaji wa mazao nje hivyo kuingiza fedha za kigeni, ni moja ya
vigezo vya kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania.
Kwamba, nchi
imekuwa ikiagiza zaidi nje kwa kutumia dola ya kimarekani kuliko inavyouza,
jambo ambalo lingeweza kupunguzwa kwa kuwekeza katika kilimo ambacho
kingeboresha uchumi wa wakulima hadi taifa.
Wakati hali
ikiwa hivyo kwa Tanzania, hali ni tofauti nchini China ambapo kilimo kimejengewa
mazingira bora kiasi cha kuwa sehemu ya utalii.
Mwandishi wa
makala hii aliyekuwa miongoni mwa waandishi waliofanya ziara ya mafunzo nchini China, aliweza kujionea mengi katika
sekta hiyo ambayo imekuwa na tija kubwa kwa wakulima.
Wanahabari wajionea
mashamba ya mfano ambayo huyatumia kama sehemu ya kuwaongezea kipato wakulima.
Kwa mujibu wa
Chen Xian Juan, meneja wa shamba la mfano katika kijiji kimojawapo, anasema utalii
huo wa kilimo, umekuwa ni kivutio
kikubwa kwa wa wageni wanaofika katika mashamba hayo ya kitalii kujionea namna ya kulima kilimo cha kisasa na
chenye manufaa.
Anasema, mambo
yanayopatikana katika siku za maonyesho hayo ni pamoja na kuogelea, nyama choma
na maonyesho ya mazao yao ambayo hulimwa na wanakijiji.
Aidha, wanahabari
waliweza kushuhudia mashamba ya mfano yaliyopo vijijini na kuwaona baadhi ya
wakulima wakiendelea kutumia jembe la mkono, lakini wengine wamekuwa wakitumia
trekta pamoja na zana za kilimo za kisasa.
Juan anasema
baada ya mazao kwa mfano matunda na mbogamboga kuvunwa, hufanyiwa utafiti wa
kutosha kama yanafaa kuliwa na binadanu kabla ya kusafirishwa kupitia kwa mawakala
maalumu waliopo maeneo ya mijini kwa ajili ya kuyasambaza kwenye masoko ya miji
ya China.
Katika mji wa
Xingying, wanahabari ulishuhudia pia mazao yaliyostawi vyema kama mahindi,
maharage, viazi, magimbi, maboga, pilipili-hoho na jamii nyingine za mbogamboga
ambapo sasa wanajipanga kuanza kuuza kwa njia ya mtandao.
Je, nini siri
ya mashamba yenye rutuba?
Juan anasema
katika mji wao, wamekuwa wakijitahidi kupambana na uharibifu wa mazingira, hivyo
wako tofauti na Beijing ambako hali yake siyo nzuri kutokana na kuharibiwa na utitiri
wa viwanda.
“Hali ya hewa
kwetu (Xingying) ni nzuri na iko tofauti na mji wa Beijing kwani mazingira yake
yameharibiwa na viwanda na kemikali, hivyo hata ardhi yake haiwezi kumea kitu,”
anasema Juan.
Anasema, licha
ya kufanikiwa kutunza mazingira ya eneo hilo, pia hutumia mbolea ya asili kwa
mfano kinyesi cha wanyama kwa ajili ya kuongeza ubora wa mazao mashambani.
0 Comments