Naibu Waziri Wa Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Stanslaus Nyongo ame toa rai kwa Viongozi wa Mkoa wa Pwani kuendelea kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwa usahihi ndani na nje ya nchi.
"Wawekezaji wapewe maelezo sahihi na taarifa muhimu za ardhi zilizokuwa za kweli kwa sababu zitasaidia kukaribisha uwekezaji ,vivo hivyo Mikoa mingine nao wanaowajibu wa kutoa taarifa za kweli ili kuhamasisha na kuvutia wawekezaji"
amesema Mhe. Nyongo.
Naibu Waziri huyo amesema hayo tarehe 18 Desemba alipokuwa akifungua Kongamano la siku moja la Maonesho ya Wiki ya Viwanda biashara na uwekezaji Mkoani Pwani lililofanyika kwenye Ukumbi wa mikutano wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere iliyopo Kwamfipa Kibaha.
Mhe.Nyongo
amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa katika uboreshaji wa sera za uwekezaji kwa kuanzisha Wizara maalum ya Mipango na Uwekezaji ambayo ipo chini ya Ofisi yake.
Aidha Nyongo ametoa pongezi kwa viongozi wa Mkoa wa Pwani kutokana na kuutangaza vema Mkoa hasa kwenye sekta ya viwanda na uwekezaji.
Kuhusu mada ya uwekezaji katika uchumi wa buluu imeelezwa kuwa ni jukumu la viongozi wa Mkoa wa Pwani kukuza uchumi wa buluu ikiwa ni pamoja na kuzitumia fukwe kuzitengeneza kuwa rafiki kwa wakazi wake pamoja na watalii kwenda kuzitumia kwa maendeleo ya kiuchumi, michezo mbalimbali.
Mkuu wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Prof Marcellina Chijoriga. Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe Abubakari Kunenge amesema anamshukuru Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt.Selemani Jafo kwa kuyapandisha hadhi maonesho hayo jana na kutokana na mamlaka aliyonayo kuwa kuanzia mwakani yatakuwa yakifanyika Kitaifa ni jambo la kujivunia sana.
RC Kunenge alitoa fursa kwa mgeni rasmi kuangalia picha mjongeo ambazo zilionesha fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana ndani ya Mkoa wa Pwani.
Amesema kuwa kuwa majadiliano ndani ya Kongamano hilo yatatumika kama mojawapo ya nyenzo katika kukuza uwekezaji ndani ya Mkoa wa Pwani.
"Mkoa wa Pwani una hali ya hewa nzuri katika kuvutia wawekezaji ikiwemo miundombinu zikiwemo Barabara, umeme na maji.
RC kunenge amesema kuwa hivi sasa Mkoa unajipanga kwenye kuwekeza katika utalii wa baharini ikiwamo kukuza uchumi wa buluu.
Akizungumza kuhusu changamoto wanazokabiliana nazo kwenye kukuza uchumi wa buluu
amesema kuwa visiwa vingi hasa vilivyoko Wilayani Mafia vinamilikiwa na watu binafsi tofauti na inavyodhaniwa lakini kwa eneo chache lililobaki Mkoa umeshapima eneo hilo na tayari kwa kuliandaa kiutalii huku lengo likiwa kukuza uchumi wa buluu.
Kongamano hilo la Wiki ya maonesho ya viwanda biashara na uwekezaji Mkoani Pwani limefanyika kwa mara ya nne na limehudhuriwa na wakuu wa Wilaya zote za Mkoa wa Pwani Kamati ya Ulinzi na Usalama, Wakurugenzi wote wa Halmashauri zote, Wakuu wa Idara , Viongozi wa Siasa na wananchi wa kawaida.
0 Comments