Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt Rogers Jacob Shemwelekwa ametoa onyo kali kwa wapangaji wa maduka ambao wamepanga kwa lengo la kuwa madalali kuwa watachukuliwa hatua stahiki kutokana na kwenda kinyume na maombi yao ya kuwa wapangaji.
"Natoa onyo kwa wapangaji ambao wameomba na kupatiwa nafasi kwenye soko letu jipya na la kisasa Kibaha Shopping Mall kwamba tutafuatilia aliye panga ndiye anayetakiwa kufanya biashara na siyo kinyume cha hapo, hakuna udalali kwenye maduka yetu kama mtu akibainika anakuwa dalali tutamshughulikia mara moja pindi itakapo bainika" amesema Mkurugenzi Shemwelekwa.
Shemwelekwa amesema kuwa kwa kupitia soko hilo la kisasa wanatarajia kukuza ukusanyaji wa mapato ya ndani ,huku yatasaidia kwenye kununua madawa ,madawati , kujenga shule, zahanati na barabara ndani ya Kibaha.
Soko hilo la kisasa limezinduliwa leo tarehe 7 Desemba, 2024 na Mkuu wa Wilaya Kibaha Nickson Simon ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Msanii Jay Melody akitumbuiza wakati wa uzinduzi wa Soko hilo la kisasa Kibaha Shopping Mall na Msanii mzawa msanii wa Kibaha Smata.
Wakati huohuo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt. Rogers Jacob Shemwelekwa amesema kuwa ndani ya miaka mitatu ijayo mapato ya ndani yatakua maradufu kwa sababu wanategemea kukusanya zaidi ya Bil.15 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri ya Mji Kibaha.
"Kutokana na fedha za mapato yetu ya ndani tumeweza kuchonga barabara ,kujenga shule ya mchepuo wa Kiingereza na tumenunua eneo la maegesho Misugusugu" amesema Dkt.Shemwelekwa.
"Ujenzi wa soko hili umegharimu kiasi cha Bil.8 fedha ambazo zimetoka serikali kuu" amesema Shemwelekwa.
Aidha ameongeza kwa kusema kuwa huduma zinazopatikana ndani ya soko hilo kuwa wamo wafanyabiashara wenye nembo zote kubwa,huduma za benki, kuna sehemu imetengwa kwa ajili ya michezo ya watoto,sehemu za kuuza vyakula na vinywaji
mbalimbali (bar).
"Huu ni mradi wa kimkakati pia matarajio yetu ni kukusanya kiasi cha Mil.660 kwa mwaka" anesema Dkt.Shemwelekwa.
Leo ni siku ya burudani na biashara kwa wakaazi wa Kibaha na viunga vilivyopo jirani pia ikumbukwe kuwa safari ya ujenzi wa soko hili ilianza mwaka 2018 na kukamilika sasa hivyo nampongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha , Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kibaha Mwajuma Nyamka,Mbunge Silvestry Koka Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Kibaha wote hawa wamechangia kufanikisha safari hii.
"Kuna fedha kidogo zimebaki tutajenga soko la wajasiriamali wadogo pembeni na tutawawekea mazingira rafiki ya biashara" amesema DC Nickson.
0 Comments