RAIS WA ZANZIBAR DKT. SHEIN KUWA MGENI RASMI TUZO ZA TASWA


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohammed Shein anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika utoaji wa tuzo za Wanamichezo Bora Tanzania Ijumaa wiki hii.
Tuzo hizo zinaandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) na mwaka huu zimedhaminiwa na Selcom Wireless, Said Salim Bakhresa & Co Ltd - Bakhresa Group, IPTL, mifuko ya hifadhi ya jamii, PSPF na NSSF.
TASWA inaishukuru Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano wake na kukubali Rais Dk. Shein aje katika tuzo zetu, ambazo zitafanyika ukumbi wa Diamond Jubilee, VIP Dar es Salaam.
Kukubali kwa Dk. Shein kuwa mgeni rasmi kunaonesha jinsi gani alivyokuwa mwanamichezo wa kweli na mwenye nia ya dhati ya kushirikiana na wadau wa michezo nchini.
Katibu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) Amir Mhando (kulia) akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kuhusu tuzo za TASWA zinazotarajiwa kufanyika jumamosi hii katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Katikati ni Makamu Mwenyekiti wa TASWA, Egbert Mkoko na mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Mwani Nyangasa 
******************************
Wanamichezo 44 wanatarajiwa kupewa tuzo siku hiyo baada ya kufanya vizuri katika michezo mbalimbali kuanzia Juni 2013 hadi Juni 2014. Pia itatolewa Tuzo ya Mwanamichezo Bora wa jumla na Tuzo ya Heshima.
TASWA imewahi kutoa Tuzo ya Heshima kwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa, pia imewahi kutoa Tuzo ya Heshima kwa timu ya soka ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ iliyokuwa ikicheza mechi za kufuzu fainali za mataifa ya Afrika mwaka 1980 zilizofanyika Lagos, Nigeria.
Tunaamini zitakuwa tuzo za aina yake, ambapo tayari Kamati ya Kusimamia Tuzo hizo imeshatangaza majina ya wanamichezo zaidi ya 100 wanaowania tuzo mbalimbali.

Post a Comment

0 Comments