BAADHI YA WAHARIRI KUTOKA KATIKA VYOMBO MBALIMBALI VYA HABARI WAKIBEBA JENEZA LA MAREHEMU WILLY EDWARD OGUNDE ULIOAGWA KATIKA VIWANJA VYA MNAZI MMOJA DAR ES SALAAM, MWILI HUO UMESAFIRISHWA LEO MCHANA KWENDA NYUMBANI KWAO MUGUMU MUSOMA MKOANI MARA.
WANAHABARI WANASIASA WAMLILIA.
NILIKULA CHAKULA CHA MWISHO NA WILLY
Na Martin Malera
SAA chache kabla ya kifo chake, nilikula chakula cha jioni na Willy Edward bila kujua kama ilikuwa kalamu yake ya mwisho.
Wote tulikuwa kwenye mkutano wa wahariri wa vyombo vya habari mjini Morogoro kujadili maandalizi ya Sensa.
Mwisho wa semina majira ya saa 10, washiriki wote tulienda kupata chakula tulichopaswa kula mchana, lakini tuliamua kumaliza shughuli zote za semina kisha tupate chakula cha mchana bila kujali muda.
Mimi na Willy ambaye alipata kuwa msimamizi wangu wa harusi miaka tisa iliyopita, tulikaa meza moja.
Tulipomaliza chakula, washiriki wote waliondoka. Mimi na Willy tulibaki pale pale na kwenye meza ile ile tukibadilishana mawazo.
Tuliagiza mahindi ya kuchemsha. Nilichukua mhindi wa kwanza, tukakatiana. Ulivyoisha, Willy naye alichukua mhindi mwingine, nao tuliushambulia kwa kukatiana. Tulifurahia sana.
Tukiwa tunatafuna mahindi, Willy aliniambia “Martin, nimeshiba. Huu ndio msosi wangu wa mwisho, sihitaji tena chakula leo,”. Nilibaki kumwangalia tu.
Aliniambia anataka kuzungumza na watoto wangu anaowajua vyema. Alifurahi sana kuwasikia Winni na Fred. Akaniambia Kaka, naona unakuza. Kisha akapiga simu kwa mkewe ambaye sasa ni mjane, Rehema Edward (Mama Colin). Akanipa simu nizungumze naye. Nilizungumza naye kwa utani na kila mtu alifurahia.
Mimi na Willy Tulizungumza mengi kuhusu namna bora ya kutunza na kulea familia zetu kwa kuhakikisha wanapata elimu bora.
Tulijadili masuala kadhaa ya soka wote tukiwa wanazi wa kutupwa wa Yanga. Tuliumizwa na jinsi Yanga inavyowekeza kwenye migogoro badala ya soka. Hakika tulipata muda mzuri wa majadiliano.
Giza kilianza kuingia majira ya saa moja kama na nusu, mimi na willy tuliendelea kubaki pale wakati wenzetu, baadhi walirejea Dar na wengine walienda kwenye nyumba za kulala wageni walizofikia.
Tuliamua kuhamia kwenye baa moja iliyojirani na stendi kuu ya mabasi ya Msamvu kwani nilikuwa na mpango wa kurudi Dar es Salaam wakati Willy akinitaka nilale Morogoro.
Mwisho wa siku kila mmoja alibaki na msimamo wake.
Mshituko.
Majira ya saa nane usiku nilipigiwa simu na mkewe akilia na kuhoji kimetokea nini kwa Willy. Sikuwa na majibu zaidi ya mshangao
Naandika makala hii kumlilia Willy ambaye leo tumemuaga hapa viwanja vya Anatoglo Mnazi mmoja. Willy ametoweka. hatarudi. Ametoweka kimwili. Kiroho daima atakuwapo. Atakuwapo kama darasa la maisha. Atakuwapo kama darasa hasa katika tasnia ya habari.
Nitatoa sababu: Willy ni darasa kwani mbali ya kuwa mwandishi, pia ni msanifu kurasa. Katika habari Willy ni ‘Jembe’ kwani ni mwandishi wa habari za michezo na wakati huohuo ni mwandishi wa habari ngumu.
Ndiyo maana naendelea kumlilia na kutamani kilichotokea kisingetokea. Lakini wapi. Maana hukumu ya Mungu haina rufani. Na isitoshe ni sehemu ya malimwengu yenye rangi rangile.
Willy ameondoka na deni. Deni alilokuwa tayari kulilipa. Yaani kutimiza wajibu wake kupitia kalamu kwa kuwaanika hadharani vigogo wa ufisadi ambao majina yao yananuka kuliko hata uoza.
Je kweli tulimpenda willy au tumempenda baada ya mauti kumfika? Jukwaa la Wahariri tulimpenda Willy? Nina mashaka.
Leo amefumba macho tunazidisha mapenzi!
Tangulia Jembe, dunia waachie wanaojiona ni wenyewe japo wanajidanganya kwani sote tu wapita njia.
Wewe nenda salama. Umetuachia mtihani wa kumalizia kazi yako ya kulipa deni. Ewe nenda mwanakwetu wenye kufurahi wafurahi. Japo siyo jibu wala njia kwani nao ipo siku yao. Nani alijua? Ni nani alijua? Nani alijua Willy kama ungeondoka kwa staili aliyoondokea jamani?
Umeondoka na siri. Maana uliwatanguliza wanao Morogoro, kisha ukawafuata kuwaaga bila hata ya kumuaga mkeo. Nenda. mwana kwetu nasi ipo siku tutakufuata.
Willy Jembe, jiendee mwanakwetu umetimiza wajibu wako. Willy tulikupenda nawe ukatupenda. Wanamichezo walikupenda, wanamuziki walikupenda, wanasiasa walikupenda, wafanyakazi wenzio wa Jambo Conserpt walikupenda, lakini familia yako yenye watoto wadogo, ilikupenda zaidi.
Nenda willy umeondoka na sifa njema kama manukato huku ukiwaachia unongo waliokudharau na kukupuuzia kwa kila jambo.
Nenda mwanakwetu, nenda jembe usisimame wala kugeuka nyuma. Nenda tuachie sisi kwani hatujui siku yetu. Nenda willy ujue tulikupenda, lakini Mungu amekupenda zaidi. Unaacha nyuma mke na watoto wako. Inauma sana.
0713260071
0 Comments