Na Salehe Mohamed
“SALEHE ndugu yangu usiwe na wasiwasi leseni ya udereva utaipata wiki ijayo, Jumatatu (jana) nitakupeleka kwa rafiki yangu ambaye ni trafiki akusaidie njia za kuipata”.
“Si vizuri kuendesha gari bila ya kuwa na leseni, ajali ikitokea utapata matatizo makubwa zaidi, mimi leseni yangu imekwisha na nimefanya taratibu za kuihuisha, Jumatatu nitaipata mpya”.
Hiyo ilikuwa ahadi ya rafiki yangu marehemu Willy Edward aliyonipa Ijumaa jioni (Juni 15) pale mkoani Mororogo baada ya kumueleza kuwa nimechoka kuendesha gari bila ya kuwa na leseni ya udereva.
Ahadi hiyo hakuweza kuitimiza kwani mimi ndiye niliyeubeba mwili wake kutoka chumba cha kuhifadhia maiti pale Morogoro na kuushusha katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Hivi ndivyo kazi ya Mungu ilivyochukua mkondo wake, hatukujua lililopo mbele yetu sisi tulichokijua ni kupanga mipango yetu kulingana na upeo tulionao.
Willy amekutwa na mauti akiwa mkoani Morogoro ambako tulikwenda kuhudhuria semina kuhusu maandalizi ya zoezi la kuhesabu watu na makazi (sensa) na umuhimu wa zoezi hilo iliyoandaliwa na Ofisi ya Takwimu ya Taifa.
Wakati wa semina mimi na yeye tulikaa mwishoni mwa ukumbi ambapo ilikuwa ni jirani na mlango wa kuingia msalani .
Willy aliniambia ‘hii ndiyo faida ya kuchelewa kufika ukumbini, sasa zoezi tulionalo mbele yetu ni kuwafanyia sensa watu wanaoingia huku maliwatoni na mwisho wa siku tuwape takwimu zao”
Jarome Risasi kutoka Redio Clouds, ndiye aliyelikuwa mtu wa kwanza kuingia maliwatoni kabla ya kuufungua mlangoni tulimwambia sisi tunafanya sensa ya wanaoingia msalani .
Nakumbuka wakati tumemaliza semina Jarome aliingia tena maliwatoni na alipotoka tulimwambia yeye amevunja rekodi kwa kuingia mara tatu, akatujibu kweli kazi hiyo imetufaa tumeifanya kwa umakini mkubwa, sote tulicheka .
Baada ya kupata somo la Sensa, Willy alinitania “ Salehe nina uhakika siku ya Sensa (Agosti 26), utahesabiwa ukiwa Gesti ambayo sijui itakuwa mkoa gani, mke wako atakuwa mkuu wa kaya yako kule Dar es salaam ”
Utani huo aliufanya tena kwa kunisisitiza kuwa sitakuwa na haja ya kuhojiwa kwani karani wa kuhesabu akifika chumba nilicholala nitampa karatasi iliyojazwa kila kitu.
Aliniambia hivyo kwakuwa kwenye semina hiyo tuligawiwa nyaraka nyingi zitakazotumika kwenye zoezi hilo na tulishiriki kwenye zoezi la mfano wa kuzijaza.
Utani huu kamwe sitousahau, sikujua kama alikuwa akiniaga, laiti angeniambia ndiyo ilikuwa siku yake ya mwisho ningemzuia asiende kuwaona watoto wake.
Baada ya semina ile Willy aliniuliza swali la uchokozi “Leo hii unarudi Dar? Kwani hujapata nyumba ndogo ya kulala nayo ili utumie fedha uliyopewa kwenye semina?”
Nilimjibu “Mimi lazima nilale hapa Morogoro kwasababu mama yangu, bibi yangu, kaka yangu na ndugu zangu wengi wanaishi hapo, nitalala, kula, kuoga bure”
“Mimi si kama wewe Willy, nina hakika unalala hapa kwasababu umeshapata nyumba ndogo”
Willy alitoa kicheko cha kebehi, akanijibu kuwa Morogoro ana ndugu wengi sana, akaongeza kuwa watoto wake watatu wanaishi eneo la Forest kwa baba yao mkubwa na baadae atakwenda kuwaona.
Baada ya hapo tulikwenda kula na baadae tuliachana na Willy majira ya saa 11 jioni, huku tukipeana ahadi ya kukutana jana (jumatatu) ili anisaidie mchakato wa kupata leseni.
Asubuhi ya Jumamosi (Juni 16), nilishtushwa na ujumbe mfupi wa simu ya mkononi kutoka mhariri wenzangu wa gazeti la Mtanzania, Kulwa Karedia akinihoji kwanini sipokei simu yake tangu saa 9 usiku alikuwa akinipigia kuniarifu matatizo yaliyompata Willy.
Nilikurupuka kitandani na kukaa sawa, nikampigia simu na ndipo aliponiambia Willy amefariki, nilipigwa na butwaa nisijue la kufanya.
Baada ya muda nilimuuliza tunafanyaje hasa kwakuwa wahariri tuliobaki mkoani Morogoro kwa wakati huo tulikuwa mimi na yeye, akaniambia tukutane BP ya Msamvu kwa ajili ya kwenda Mochwari.
Wakati wote huo nilikuwa siamini kama Willy anaweza kufa kirahisi namna hiyo huku akiwa hajatimiza ahadi ya kunitafutia leseni ya udereva.
Nilipokutana na Kulwa aliniambia lile aliloniambia Willy kuwa anakwenda kuwaona watoto wake ndiyo alikuwa akienda kuwaaga kwani baada ya hapo umauti ulimfika
Maelezo hayo ya Kulwa hayakunifanya niamini kuwa mwenzetu huyo amefariki, njia nzima nilikuwa nikiwaza mazungumzo yetu na marehemu siku iliyopita.
Nilipofika Mochwari ndipo nilipoamini Willy amefariki, nilimsemesha hakuitikia, nilimshika hakushtuka. Sura ya nuru na ucheshi aliyokuwa nayo ilizimika. Hakuwa yule aliyeniahidi kunitafutia leseni ya udereva.
Baada ya tulianza kufanya taratibu za kuuandaa mwili wake kwa lengo la kuusafirisha hadi Dar es salaam, wakati huo wote nilikuwa nikitafakari uwezo wa Mungu wa kutoa na kumpa mtu pumzi.
Wakati huo wote akili hazikuukubali ukweli kuwa Willy amekufa, mama mdogo wa marehemu aliniambia Jumamosi usiku marehemu alifika nyumbani kwake eneo la Forest na kuzungumza na watoto wake.
Anasema mazungumzo hayo pia yalichanganyika na utoaji elimu ambapo Willy alikuwa akiwafundisha mpaka pale watoto wake walipomueleza kuwa wamechoka na wanataka kwenda kulala.
Walimuambia kuwa huo ulikuwa ni usiku mwingi na wangependa kupumzisha miili yao, Willy alikubalina na uamuzi wao akawaaga kwa mara ya mwisho bila wao kujijua.
Baada ya kuagana na watoto wake, mama yake mdogo alimpigia simu dereva wa pikipiki (boda boda) ili amrudishe marehemu hoteli aliyofikia ya White House.
Willy hakuweza kupanda pikipiki hiyo kwani alianza kujisikia vibaya na kushika sehemu ya kifua kama wafanyavyo watu wasikiao maumivu makali ya moyo.
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa safari ya umauti kwani alianguka chali na sehemu yake ya nyuma ya kichwa iligonga ardhini.
Wakati huo wote dereva bodaboda alikuwa kama vile yupo ndotoni, alipogutuka aliamua kukimbilia mlangoni kwa mama yake mdogo marehemu ambapo aliwaarifu kuwa ndugu yao ameangua.
Mama yake na ndugu wengine walipofika eneo la tukio walimbeba Willy huku wakiwa na matumaini kuwa amezimia, waliamua kwenda kwenye hoteli alikufikia ili wamchukulie dawa alizokuwa akitumia.
Kumbe Willy alikuwa na matatizo kwenye mishipa yake ya kufikisha damu kwenye moyo, tatizo hilo lilimfanya apewe dawa alizokuwa akizitumia kila wakati kulingana na hali yake pamoja na maelekezo ya daktari.
Kwa mujibu wa mama yake mdogo mlinzi wa hoteli hiyo hakuwafungulia licha ya kugonga sana ndipo walipoamua kumkimbiza hospitali ambapo walipomfikisha mapokezi walipatwa na mshtuko mkubwa.
Mshtuko huo ni kuwa mgonjwa waliyemleta alikuwa ameshafariki, hilo lilikuwa pigo kwa familia na tansia ya wanahabari.
Kimsingi safari ya Willy inatupa somo sisi tuliobaki kuwa tuishi kwa ushirikiano, upendo na kumuabudu Mungu maana hatujui lini mauti yatatufika
Tuna kila sababu ya uiga mazuri yote aliyoyafanya na kuyaacha mabaya, hakuna binadamu aliyekamilika, tumuombee mwenzetu alale pema peponi.
Tangulia Willy, ila nakuahidi leseni ya udereva nitaipata wiki hii kama ulivyoniahidi ingawa sijui nani atanisaidia, kalale pema peponi….Amin.
0 Comments