Na Aristide Kwizela (BASATA)
Msanii mahiri wa mashairi nchini,Mrisho Mpoto pichani ameeleza kile anachoamini kwamba,tasnia ya sanaa na wasanii wa Bongo hawawezi kamwe kupata mafanikio katika ngazi ya kimataifa kutokana na ulimbukeni wa kuiga sanaa za watu wengine, kudharau asili yao na kujipachika usupastaa wa kubumba.
Mpoto aliyasema hayo wakati akiwasilisha mada yake iliyohusu Muziki wa Asili na Mashairi kwenye Jukwaa la Sanaa Jumatatu hii ambapo alisisitiza kwamba,wasanii wa bongo wamekuwa ni wa kulalama na kulia njaa kutokana na kazi wanazozalisha kushindwa kabisa kupata mvuto wa kimataifa na kushindana kwani zimekuwa kwa asilimia kubwa zikifanana na tamaduni za nje hivyo kukosa jipya.
Akijitolea mfano yeye mwenyewe Mpoto alisema kwamba, ameweza kukaa chini na kubuni sanaa ya asili ya Tanzania ambapo amekuwa akighani mashairi na kuyaweka kwenye mdundo wa muziki na hivyo kupendwa na idadi kubwa ya watanzania na kupenya kimataifa hivyo kumfanya kupata mialiko na fursa nyingi za fedha ambazo zimekuwa zikimpatia mafanikio makubwa.
Kwake yeye Mpoto anaamini kwamba, Sanaa ya Tanzania na wasanii wake hawaonekani kugundua siri ya kufanya kazi za sanaa zenye asili yao na badala yake wamekuwa makasuku wa kujifananisha na kuishi maisha kama ya Ulaya na Marekani huku kazi zao zikifanana kila kitu na hizo za nje hali ambayo imeifanya sanaa kupwaya na wasanii wenyewe kuishi maisha ya njaa.
Aliongeza kwamba, ni ngumu kupata msanii wa bongo anayefanya sanaa peke yake kwani mara nyingi lazima wachanganye na shughuli zingine ili kupata kipato kutokana na kazi zao kutowalipa.Katika hili Mpoto anaamini kwa kiasi kikubwa limesababishwa na wasanii wenyewe kukosa ubunifu, kuiga kila kitu kutoka nje, kulewa sifa za mapema, kukumbatia sanaa zisizo za asili yao na kujipachika usupastaa wa kubumba.
“Nimekuwa nikipata mialiko mingi nje ya nchi,siku chache zijazo nitaenda Denmark,Finland,Ufaransa, na Uholanzi.Si kwa kuwa napendwa sana bali ni aina ya sanaa ninayofanya ina asili yangu ya Tanzania na inanitambulisha kila ninakokwenda.Waache wasanii wengine wavae nguo chini ya makalio yao au hata watembee uchi mimi nitabaki na magunia yangu.Hili ndilo naamini litaweza kunipa mafanikio na ninayapata” alisisitiza Mpoto.
Mpoto ambaye kwa sasa ni msanii pekee aliyepata mafanikio makubwa kutokana na kupata mikataba mingi ya matangazo, mauzo ya kazi zake na mialiko ya kimataifa kutokana na kukumbatia sanaa ya asili aliwashauri wasanii wa bongo kuacha kunakiri (kukopi) sanaa za nje na badala yake wakune vichwa katika kubeba sanaa ya asili ambayo hapana shaka itawatambulisha kimataifa na kuwapa mikataba minono ya ndani na ya nje.
Mpoto aliyekuwa ameambatana na muimbaji wake wa Mjomba Band,Ismail alisema kwamba, inatia aibu na kinyaa unapoangalia sanaa za bongo kwani zinaonekana kuandaliwa na watu wenye njaa, wanaosaka fedha za fastafasta kuliko kujali nini wanapeleka sokoni hali ambayo imekuwa ikiwafanya wasanii wa Tanzania waonekane ni wa hovyohovyo, wa kudharaulika na wasio na mkakati wa kufikia mafanikio ya kisanaa.
“Kuna watu wamefanya sanaa miaka nenda miaka rudi lakini hawapigi hatua.Wamekuwa ni watu wa kulalamika bila kuzingatia ni kwa kiwango gani sanaa zao zina ubunifu na kubeba asili na utambulisho wao.Ndugu zangu tusipozingatia haya mafaniko tutayasikia tu na tutakuwa watu wa kuganga njaa na kupiga mizinga ya vocha” alimalizia Mpoto.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE YA NORWAY ARIDHISHWA NA MAANDALIZI YA MRADI LNG
-
Mkuu wa Mkoa wa Lindi Zainab Telack amekutana na Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje ya Norway Mhe.Andrea Motzfeldt Kravik na ujumbe wake akiwemo Balozi wa
Norw...
1 hour ago
0 Comments