WASANII WA BONGO WAOMBA UCHAGUZI MKUU KESHO UWE WENYE AMANI MUNGU IBARIKI TANZANIA

JOHN KITIME : Ewe Mwenyezi Mungu, tunakuomba utuongoze katika uchaguzi huu mkuu tuwaepuke wale wagombea wote wenye dalili za uchochezi, tupate viongozi wema kwa manufaa ya taifa.
ISIHAKA KIBENE : Tunaomba Mungu atufanye tuwe na amani na utulivu katika kipindi hiki cha uchaguzi, tukubaliane na matokeo yoyote huku tukimchulia kiongozi atakayepita kuwa ndie baba yetu.
JACOB STEPHEN ‘JB’: Mungu baba tazama Tanzania yako, umeiwekea mkono wako wenye nguvu siku nyingi na kuonekana ni kisiwa cha amani. Unapozungumzia amani duniani Tanzania ni mfano wake, bariki uchaguzi mkuu huu amani iendelee kutawala, shetani asipate nafasi. Ninaomba katika jina la yesu kristo Amen.
PRINCE MUUMIN MWINJUMA : Ewe Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi, naamini wewe ndiye unayepaswa kuabudiwa kwa haki na kuombwa mazuri na mabaya, nami naomba kwako mazuri kwa niaba ya Watanzania wote. Tunakuomba utujaalie amani, utulivu na upendo wa kweli baina yetu wakati huu tukielekea kwenye uchaguzi mkuu na baada ya uchaguzi pia, ewe Mola tunakuomba tutilie wepesi kutakapokuwa na ugumu. Amin.
SAID FELLA : sisi vijana tujitokeze tukapiga kura kumchagua kiongozi atakayetufaa, Mungu atuongoze tuishi kwa amani hata baada ya uchaguzi, na hao waangalizi wa Kimataifa waliokuja wakae na kuondoka kwa amani.
STEVEN KANUMBA : Amani ni jambo tunalotakiwa kulienzi na kulikumbatia mno katika kipindi hiki tunapoelekea uchaguzi mkuu kwani shetani huwa hachezi mbali, Mungu ibariki nchi yangu. Amen.
Baada ya wadau kusema hayo kila mtu yamemwingia barabara akilini na nahisi sina cha kuongeza zaidi ya kuungana nao kuuombea uchaguzi wetu uwe huru wa haki na uliojaa amani ili tuendelee kuishi salama hata baada ya matokeo ya kura zetu.
IRENE UWOYA : Tudumishe amani tuliyoachiwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika kipindi hiki cha uchaguzi jamani na hata hapo baadaye.
20%: Naiombea Tanzania isimwage damu, ndio maana siku ya uchaguzi naenda kupigia kura nyumbani Kimanzichana kusikokuwa na vurugu, lakini wapiga kura muwe na maamuzi sahihi.
LADY JAYDEE : Mungu ibariki Tanzania na Watanzania wote, uchaguzi wa viongozi uende kwa amani na upendo, kadhalika nawakaribisha wote Thai Village, Masaki jioni ya Jumapili ya uchaguzi kuburudika na Machozi Band.
MZEE YUSSUF ‘Mfalme’: Mungu alete kheri katika uchaguzi wetu, uwe ni uchaguzi huru wenye haki, amani na maelewano kwetu sote. Amin.
AFANDE SELE : Mungu wetu muweza wa yote, awape mioyo safi viongozi wa tume ya uchaguzi ili wasimame katika haki kwa kumtangaza mshindi aliyechaguliwa na wengi kihalali.

Sababu sauti ya wengi ndiyo sauti ya Mungu mwenyewe, atusimamie Watanzania tuweze kuvumiliana baada ya uchaguzi kwa kuheshimu matokeo yatakayozingatia haki na ukweli ili amani ya taifa letu iendelee kudumu.

Nasema hivi kwa sababu historia inaonyesha kwamba katika nchi nyingi barani Afrika amani yake huvunjika wakati wa uchaguzi kwa kutotenda haki dhidi ya chaguo la wapiga kura mfano; Kenya, Zimbabwe na kwingineko.

Mungu wetu ni Mungu wa haki na pasipokuwa na haki, ataliacha taifa mikononi mwa shetani ambaye ndiye baba wa machafuko. Vilio, vita na mabalaa yote yataivamia nchi yetu pendwa.
Wote hawa kesho watapiga kura huku kila mmoja akimchagua yule nayeona anafaa kushika hatamu ya nchi.Hayo ndiyo maoni ya wasanii wa hapa Bongo hivyo ni jukumu letu Watanzania wote kufanya uchaguzi wa amani usioangalia udini na ukabila kwani Amani tuliyonayo Tanzania ni tamu sanaaaaa ilinde ikulinde. Wanausalama nao wako makini hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kulina amani yake fuata maelekezo ya uchaguzi, usijionyeshe unashabikia chama gani usivae wala kujinakshi kwa rangi za chama fulani washawasa atafanya kazi yake.
Fanya fujo uone kama hutoleta ubazazi kamwe dhahmayoyote haitokukuta.

Post a Comment

1 Comments

Unknown said…
Mungu ibariki Tanzania katika uchaguzi huu. Uchaguzi ufanyike kwa usalama na umalizike kwa usalama. S.K.