KUTOKA KUSHOTO NI MENEJA WA LABEL YA MAISHA KWAME MCHAURU ANAYEFUATA NI KAROLA KINASHA NA HARDMAD
Uzinduzi wa albamu ya Maisha Lounge Vol 1 umepangwa kufanyika Ijumaa Iktoba 22 kuanzia saa 12 jioni hadi saa 3 usiku katika ukumbi wa Waterfront zamani ulifahamika kwa jina la Mashua uliopo katika Hoteli ya Sleepway Masaki Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza leo asubuhi katika mkutano na waandishi wa habari Kwame Mchauru ambaye ni Meneja wa Label ya Maisha Music alisema, albamu hii ni toleo la kwanza katika mtiririko wa matokeo mengine mbalimbali yanayotarajiwa kuandaliwa katika siku zijazo. Albamu hii ni mchanganyiko wa nyimbo tofauti na tulivu ambazo zimerekodiwa kwa vionjo vya ki- elektroniki na kuchanganywa na ladha za ala za asili za Kitanzania kama vile Ngoma, Zeze, Chalimba na Marimba. Pia albamu hii imeshirikisha wasanii wa staili tofauti tofauti ili kufanya mseto wenye kukidhi hisia za walio wengi.
Lounge ni aina ya muziki wa taratibu ambao unatumika katika maeneo mengi duniani hususan katika mahoteli makubwa na hata katika baadhi ya maofisi.Ni aina ya muziki ambao huweza kukufariji na kukusaidia katika kuleta utulivu wa mwili na mawazo.
Baada ya kuona kuwa aina ya muziki wa Lounge unaotumika hapa nchini Tanzania ni ule unaotoka katika mataifa mengine, ndipo wazo la kurekodi albamu hii likazaliwa.Hii ni kwa kutaka nasi pia tuwe na aina inayopigwa na kuimbwa katika mahadhi tutakayojifananisha nayo kwa karibu.
Albamu hii imerekodiwa katika Studio za 41 Records na Maisha Studio chini ya Produza Jacob Poll na kuboreshwa na nchini Denmark katika Studio za C4 pamoja na Red Red.Kazi hii imefanyika chini ya usimamizi wa Kampuni ya Maisha ya hapa Dar es Salaam.
Wasanii walioshirki katika albamu hii ni pamoja na Ray C, Bi Shakila, Lord Eyes, Misoji Nkwabi, Hardmad, Carola Kinasha, Fid Q na Lufu.
Uzinduzi huu umedhaminiwa na Waterfront, Miller, Michuzi Blog na 41 Records.
0 Comments