Yanga walaani Papic kupewa kipondo

Na Dina Ismail
UONGOZI wa klabu ya soka ya Yanga umeliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumchukulia hatua kali meneja wa Kagera Sugar Mohammed Hussein, ambaye alimvamia na kumpiga kocha wa Yanga Kostadin Papic.Hussein alimpiga ngumi Papic juzi baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom baina ya timu hizo kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro na Yanga ilishinda mabao 2-0.Akizungumza na waandishi wa habari jana, Ofisa Habari wa Yanga Louis Sendeu alisema uongozi umesikitishwa na kitendo hicho kisicho cha kiungwana katika michezo.Sendeu alisema tayari wameshaandika barua TFF wakishitaki kitendo cha kiongozi huyo kuanzisha vurugu ambazo zingepelekea maafa kwa mashabiki waliohudhuria mechi hiyo.“Kwa kweli tumesikitishwa sana na kitendo alichokifanya kiongozi huyo, kwa kweli si cha kukifumbia macho, kama kiongozi anaonesha utovu wa wazi wa nidhamu je wachezaji watajifunza nini?, Alihoji Sendeu.Sendeu aliongeza kwamba kiongozi huyo alionyesha dalili za ugomvi tangu kipindi cha mapumziko ambapo Yanga ilikwenda ikiongoza bao 1-0 huku kiongozi huyo alimfuata kocha wa Yanga na kumtolea lugha chafu.Aidha, Sendeu alisema kuwa mwamuzi wa pambano hilo hakuitendea haki kwani pamoja na wachezaji wao kuchezewa rafu hakutoa kadi wa wapinzani wao, pia kuwanyima mabao ya wazi zaidi ya mawili.Katika hatua nyingine Sendeu amesema kibali cha uhamisho cha kimataifa (ITC) cha mchezaji wake kutoka Ghana Kenneth Asamoh bado kinashughulikiwa na TFF ambayo inadhamana ya kuwasiliana na shirikisho la soka la kimataifa (FIFA).Alisema kuchelewa kutoka huko kumetokana na makosa madogomadogo yaliyojitokeza wakati wa kipindi cha usajili kwa kutumia mtandao ambapo maelezo ya timu aliyotokea ya Jagodina na klabu Yanga yalitofautiana hadi muda ulipomalizika.

Post a Comment

0 Comments