CHAMUDATA WAMLILIA KING KIKII

TANZIA
Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA) kinaungana na Watanzania wote hasa wapenzi wa Muziki wa Dansi kuomboleza kifo cha mwanamuziki nguli, Kikumbi Mwanza Mpango, aliyefahamika zaidi kama King Kikii, kilichotokea jijini Dar es Salaam usiku wa kuamkia Ijumaa Novemba 15, 2024 baada ya kuugua kwa muda mrefu.

 Katika maisha yake, nguli huyu amekuwa kielelezo cha umahiri katika sanaa ya muziki kwani ameacha alama isiyofutika kwenye anga la Muziki wa Dansi nchini Tanzania; na kifo chake kimewagusa wengi.

Safari yake ya muziki, iliyochukua miongo kadhaa, ilimpitisha katika bendi kadhaa zikiwemo bendi za Norvella Jazz, Orchestra Fouvette, Marquis du Zaire, Orchestra Safari Sound, Double O, Sambulumaa, Zaita Muzika, na La Capital.

Kikii alibarikiwa kuwa na uwezo mkubwa sana wa kutunga nyimbo, sauti nzuri na ya kusisimua, na uwezo wa kutawala jukwaa. Katika maisha yake ametunga nyimbo nyingi sana zilizompa umaarufu mkubwa kama vile Nimepigwa Ngwala, Kiongo, Kyembe, Yoka Mateya ya Baboti, Dora mtoto wa Dodoma, Noele Christmas, Kitoto chaanza tambaa, na Kitamba Cheupe.

Zaidi ya mafanikio yake ya kimuziki, Kikii alikuwa mshauri na mlezi wa wanamuziki wengi sana. Mapenzi yake ya muziki yalikuwa dhahiri na yalienea kote alikokwenda. Tusherehekee maisha yake na urithi wa kudumu anaouacha. Muziki wake utaendelea kusikika vizazi na vizazi, ukitukumbusha juu ya talanta yake, upendo wake, na kujitolea kwake kwa sanaa ya muziki.

CHAMUDATA inatoa pole kwa Familia ya Marehemu, Serikali, na wadau wote wa Muziki nchini kwa kuondokewa na mtu muhimu kwenye tasnia. Mungu ampumzishe mahala pema peponi mpendwa yetu Kikumbi Mwanza Mpango, King Kikii.
Amen.

Post a Comment

0 Comments