Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) kimeipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa kuunga mkono jitihada za Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha mazingira na miundombinu bora ya elimu.
Viongozi hao kutoka Makao Makuu ya Chama hicho, wamesema Manispaa ya Kibaha ndiyo Halmashauri ya kwanza kuhakikisha kero za walimu zinatatuliwa na kuisha kabisa.
Dkt Nicas amesema, serikali kuu pamoja na Halmashauri inafanya majukumu yao , na jukumu kubwa la walimu ni kuelimisha watoto hivyo wazazi pia wanatakiwa watimize majukumu ili walimu na wanafunzi wawe na mazingira mazuri ya kusoma.
Ameongeza kuwa, kwa sasa Manispaa ya Kibaha ina shule 58 za Msingi, na shule 24 za Sekondari ambapo katika hizo Shule 14 zimejengwa na Dkt Samia Suluhu Hassan ndani ya miaka minne ya utawala wake.
Aidha, amesema tayari Halmashauri imeshatenga bajeti ya kiasi cha Bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya Shule kwa wanafunzi wanaomaliza 2027, na wana mpango wa kuweka huduma ya Internet kwenye Shule zote ili waliku wasiwe wanapata changamoto ya kutuma taarifa zao sehemu mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa CWT Taifa, Mwl Shaban Ambindwile amemshukuru na kumpongeza Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha kwa kuwa na maono na kuamini bado watu wema wanaopenda elimu.
Amesema, zipo changamoto nyingi za elimu ila baada ya kusikia mikakati na mipango iliyowekwa na Manispaa ya Kibaha inaonesha ni kwa namna gani wamejipanga kuhakikisha wanatatua changamoto zote za walimu na huo ni ushindi kwa Chama cha Walimu.
Manispaa ya Kibaha kwa mwaka wa fedha 2026/2027 imetenga bilioni 4 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 174, na tayari madarasa 22 yameshakamilika huku ikitarajia mwaka wa fedha 2027/2028 kutenga kiasi kingine kwa ajili ya ujenzi wa matundu ya vyoo na samani za shule.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa CWT Taifa , Katibu wa CWT Taifa Magesa Protas, Kaimu Mwekahazina James P. Asagwile, Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani Suzane Shesha ,Mwekahazina Mstaafu wa CWT Abubakari Alawi pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka CWT Taifa.



0 Comments