Mbio za Mwenge wa Uhuru jana tarehe 6 Julai, 2026 zilliwasili Wilaya ya Ngorongoro na kukimbizwa umbali wa kilomita 386 kuzindua miradi mbalimbali ambapo pia umepita katika eneo la hifadhi ya Ngorongoro na kuangazia maajabu saba ya Ngorongoro huku watalii kutoka mataifa mbalimbali wakishuhudia.
Ukiwa katika hifadhi ya Ngorongoro kuelekea Wilaya ya Karatu watalii kutoka mataifa mbalimbali walionyesha bashasha kuona Mwenge ukipita eneo la hifadhi lenye vivutio mbalimbali ambapo tukio hilo linaashiria uwepo wa Amani, umoja na mshikamano wa Kitaifa unaotoa tumaini kwa wageni kufanya shughuli za utalii bila changamoto yoyote
Kiongozi wa Mwenge wa Uhuru Kitaifa Bw. Wazo Michael Mwang’onda ameeleza kuwa; Ngorongoro ni hifadhi yenye vivutio vingi vya utalii na hadhi za kimataifa ambapo yeye na timu ya wakimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa wanahamasisha amani,umoja na mshkamano wa kitaifa ili kwa pamoja kuletea maendeleo kupitia fedha za kigeni zinazochangiwa na idadi kubwa ya watalii wanaotembelea hifadhi za Ngorongoro na maeneo mengine ya nchi.
Watumishi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wakiongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi anayesimamia Idara ya Wanyamapori na Utafiti Vicktoria Shayo, wameshiriki mbio kupokea Mwenge wa Uhuru katika Wilaya ya Ngorongoro na kuukabidhi leo tarehe 7 Julai, 2026 katika Wilaya ya Karatu.



0 Comments