Na Tullo Chambo
Dar es Salaam. Tasnia ya michezo nchini Tanzania imeshuhudia moja ya vipindi vya misukosuko mikubwa katika historia ya Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC). Ni mnyukano wa kiuongozi uliogubikwa na mabadiliko ya kikatiba, mivutano ya kisheria, na hatimaye mzozo wa kura uliomulika taswira ya michezo ya nchi nje ya mipaka. Hata hivyo, kuingilia kati kwa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC) na Chama cha Kamati za Kitaifa za Olimpiki Afrika (ANOCA) kumeweka nukta na kurejesha heshima ya misingi ya kidemokrasia.
*Chanzo cha Shari: Katiba Ibaguayo Watu*
Mizengwe ya sakata hili ilianza Desemba 2024, wakati mabadiliko ya Katiba ya TOC yalipofanywa. Wadau wengi wa michezo walipinga mabadiliko hayo, wakidai hayakuwa na tija kwa maendeleo ya michezo, bali yalilenga kuwengua baadhi ya wagombea. Kipengele kilichozua mzozo mkubwa ni kile kilichowazuia watumishi wa umma kugombea nafasi za ujumbe wa Kamati ya Utendaji.
Kipengele hiki kilitafsiriwa kama mtego wa kisiasa uliomlenga Anthony Mtaka, ambaye ni mtumishi wa umma na mdau mkubwa wa michezo. Hatua hii ilisababisha Mtaka kuenguliwa katika mchakato wa kwanza wa uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 28 Desemba 2024 mjini Dodoma. Mchakato huo ulifutwa rasmi na Serikali kupitia Msajili wa Vyama vya Michezo siku chache kabla ya mkutano mkuu wa uchaguzi wa 28 Desemba 2024 kutokana na matumizi ya katiba hiyo ambayo haikuwa na ithibati ya msajili, na malalamiko yaliowasilishwa yaliohusu kasoro katika mchakato wa marekebisho.
*Mivutano na Shinikizo la Wadau*
Baada ya mchakato huo wa kwanza kufutwa, TOC walitangaza mchakato wa pili wa uchaguzi uliopangwa kufanyika tarehe 4 Oktoba 2025. Hata hivyo, mchakato huu nao ulikumbwa na dhoruba ambapo Serikali kupitia waziri mwenye dhamana ya michezo wa wakati huo Mhe Paramagamba Kabudi iliingilia kati tarehe 9 Septemba 2025 na kuusimamisha, baada ya kubainika kuwa TOC walikaidi maelekezo na kuendelea kutumia katiba ileile isiyo halali badala ya ile ya mwaka 2020 inayotambuliwa na iliosajiliwa na msajili. Hali hii ilionyesha wazi kuwa TOC ilikuwa imepoteza mwelekeo na uaminifu mbele ya jamii ya michezo.
Hadi kufikia mchakato wa tatu wa mwezi Aprili 2026, shinikizo kutoka kwa wadau, vyama vya michezo, na wapenzi wa Olimpiki lilizaa matunda. Serikali na IOC ziliishinikiza TOC ambayo ililazimika kuondoa vipengele hivyo vilivyotajwa kuwa vya kibaguzi kwenye katiba. Hatua hii iliwapa fursa watumishi wa umma, akiwemo Anthony Mtaka, kurejea uwanjani. Uchaguzi ulipangwa kufanyika tarehe 12 Aprili 2026 kwenye Ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, mizengwe haikuishia hapo; Kamati ya Uchaguzi ilimkata tena Anthony Mtaka tarehe 8 Aprili 2026 kwa sababu zisizo na mashiko ya kisheria wala bila kufanyiwa usaili. Hali hii ilimfanya Waziri wa Michezo, Paul Makonda, kuingilia kati na kuufuta tena mchakato huo ili kulinda haki na kuunda uongozi wa mpito.
*Muafaka wa Machozi na Jasho*
Kufuatia mkwamo huo wa Aprili 2026, kulitokea mawasiliano mazito ya pande tatu kati ya IOC, TOC, na Serikali ya Tanzania. Mazungumzo hayo yalizaa muafaka wa kihistoria: wagombea wote walioenguliwa isivyo haki walitakiwa kurejeshwa kwenye kinyang'anyiro bila masharti yoyote.
Tarehe 5 Julai 2026, uchaguzi halali ulifanyika kwenye Hoteli ya Peacock jijini Dar es Salaam. Katika sanduku la kura, wajumbe walitoa sauti zao kwa uwazi mkubwa ambapo matokeo ya nafasi ya juu yalikuwa kama ifuatavyo:
• Anthony Mtaka: Kura 29
• Henry Tandau: Kura 6
• Leonard Thadeo: Kura 1
*Wajumbe wa Mkutano Mkuu: Mashujaa wa Uzalendo na Weledi*
Katika mazingira yaliyogubikwa na hofu na shinikizo la kisiasa, wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TOC walionyesha ukomavu wa hali ya juu. Badala ya kuyumbishwa na upepo wa maslahi binafsi, wajumbe hawa waliamua kuweka mbele uzalendo na weledi ili kuiokoa TOC kwa niaba ya mamilioni ya Watanzania. Uamuzi wao wa kumpigia kura nyingi Anthony Mtaka ulikuwa ni tamko la wazi kuwa michezo haitakiwi kuchezewa. Walisimama kidete kulinda heshima ya taasisi, wakijua wazi kuwa mustakabali wa wanamichezo wa Tanzania unategemea uongozi thabiti na unaokubalika na wengi.
*Ibrahim Mkwawa na Poromoko la Uadilifu (Integrity)*
Licha ya ushindi huo wa kishindo wa Mtaka, Kamati ya Uchaguzi chini ya uenyekiti wa Ibrahim Mkwawa ilifanya kile kilichoshangaza ulimwengu wa michezo. Kamati hiyo ilitenda madudu kwa kujaribu "kupindua meza" na kumtangaza Leonard Thadeo—aliyetokea kupata kura moja tu—kuwa mshindi wa kiti cha Urais kama ilivyothibitishwa na barua ya IOC.
Hatua hii imemvua nguo Ibrahim Mkwawa mbele ya jamii. Amethibitisha kuwa ni kiongozi asiyekuwa na chembe ya uadilifu wala unyoofu wa nafsi (integrity). Kwa makusudi kabisa, Mkwawa alichagua kukiuka matakwa, sauti, na maamuzi ya kisheria ya wajumbe wa Mkutano Mkuu. Kitendo hiki cha kugeuza matokeo ya kura zilizohesabiwa hadharani hakikuwa tu ukiukwaji wa kanuni, bali kilikuwa ni usaliti mkubwa kwa taaluma yake ya sheria na uaminifu aliopewa kusimamia haki. Ninaamini, TLS hawatajisikia ufahari kua madudu haya yamefanywa na mwanachama wake.
*Kushuka kwa Heshima ya Leonard Thadeo: Kutoka Kiongozi hadi Mshiriki wa Uporaji*
Leonard Thadeo ni mtumishi wa umma mstaafu mwenye historia ya kushika nafasi mbalimbali za muhimu zenye dhamana ya usimamizi wa michezo nchini. Amekua msajili Baraza la Michezo la Taifa, Mkurugenzi wa maendeleo ya michezo nchini na mkurugenzi wa michezo TAMISEMI. Kwa kifupi kabla ya mzozo huu, Thadeo alistaafu akiwa na historia ya aina yake katika michezo nchini na kua moja ya taswira za kuaminika katika usimamizi wa michezo nchini. Hata hivyo, mzozo huu umeacha kovu kubwa zaidi kwenye wasifu wa Leonard Thadeo. Kwa kukubali kutangazwa mshindi kwa kura moja dhidi ya kura 29, Thadeo ameshusha heshima yake kwa kiwango cha chini kabisa ambacho hakijawahi kushuhudiwa. Alihalalisha uporaji wa mchana kweupe dhidi ya Anthony Mtaka na kupoteza sifa zote za kuwa kiongozi wa kiroho na kimaadili katika michezo.
Kile kilichosikitisha na kustaajabisha wengi ni kitendo chake cha kukubali kwenda kuapishwa kwa dharura tarehe 6 Julai 2026 akisindikizwa na familia yake. Katika hali ya kawaida, kiongozi mwenye uadilifu, utu na busara angetambua ubatili huo na kuukataa. Thadeo alichagua kubeba familia yake kwenda kushuhudia "sherehe ya haramu", akisherehekea ushindi usio wake, huku akijua fika kuwa anajivika joho la dhuluma mbele ya familia yake. Kama kuongeza pigo katika uso wake, hakuna kiongozi yeyote wa serikali, si kutoka wizarani, BMT, BMTZ, wala ofisi ya msajili wala Mrajisi aliehudhuria uapisho wake. Hii ikimaanisha kua serikali imeamua kujitenga kabisa na dhulma hii na kuacha sheria na taratibu za michezo zichukue mkondo wake. Kitendo hiki kimebaki kuwa alama ya aibu na dhihaka kubwa kwake na kwa kizazi chake. Hapa hekima ya wajumbe wa mkutano mkuu inaonekana katika maamuzi yao ya kumpa kura moja kati ya 36 zilizopigwa.
*Tamko la IOC na Safu Kamili ya Viongozi Walioidhinishwa*
Kitendo hiki cha kitapeli kilivutia jicho la mwangalizi huru wa kimataifa, Dk. Donald Rukare, aliyekuwa anafuatilia uchaguzi huo kwa niaba ya IOC. Kupitia barua rasmi ya tarehe 9 Julai 2026 kutoka Lausanne, Uswisi, IOC na ANOCA walilaani vikali usaliti huo, wakabatilisha sarakasi za Kamati ya Mkwawa, na kumthibitisha rasmi Anthony Mtaka kuwa Rais halali na wanaemtambua.
Pamoja na Rais Mtaka, vyombo hivyo vya kimataifa vimeidhinisha rasmi safu mpya ya viongozi na wajumbe wa Kamati ya Utendaji waliopata kura halali za wajumbe:
• Rais: Anthony John Mtaka
• Makamu wa Rais: Nassra Juma Muhammed
• Wajumbe wa Kamati ya Utendaji (Bara na Zanzibar):
1. Noorain Gulam Hussein Shariff
2. Amina Mohamed Mfaume
3. Khalid Yahya Rushaka
4. Suma Steven Mwaitenda
5. Abdulkheir Ahmed Mohammed
6. Abdulrahman Said Simai
7. Makame Ally Machano
8. Thuwaiba Aboud Muhiddin
9. Mwatima Bakari Abdi
10. Said Mohamed Abdullah
Tunasisitiza kamati iliomaliza muda wake iheshimu maelekezo ya IOC na kuyatekeleza kama yalivyo, bila hila wala janja janja kwa maslahi mapana ya nchi. Zinasikika tetesi za hapa na pale, lakini niwasihi wasikubali kuidhalilisha nchi yetu kimataifa. Heshima ya nchi kimataifa ni kubwa kuliko wao na maslahi yao binafsi, tunaomba waachie ofisi ili viongozi halali waanze kazi.
*Mapambazuko TOC*
Uongozi uliopita wa TOC pamoja na wale waliotaka kujivika madaraka kwa ubatili wameamriwa kukabidhi mali zote, ofisi, kurasa za mitandao ya kijamii, na akaunti za benki mara moja kwa uongozi huu mpya wa Mtaka.
Sakata hili la TOC linabaki kuwa somo kubwa kwa vyama vya michezo nchini Tanzania. Linatufundisha kuwa, michezo ni chombo cha haki na uwazi. Majaribio ya kutumia madaraka kuengua watu au kupora ushindi, sio tu kwamba yanalemaza michezo yetu, bali yanatia doa nchi yetu kimataifa. Tumejijengea heshima kubwa katika maendeleo ya michezo, heshima inayotupa nafasi ya kuandaa mashindano mbalimbali makubwa ya michezo ya kimataifa kwa uchache tu nataja AFCON inayotarajiwa hapo mwakani. Sauti ya wajumbe wazalendo imeshinda dhuluma, na sasa ni wakati wa Mtaka na timu yake kuivusha TOC kuelekea kizazi kipya cha heshima na ushindi. Ni wakati wa serikali na wadau wote kuwapa ushirikiano kwani safari ya kuelekea Los Angeles Olympic 2028 imekwishaanza. Mtaka na Bi Nasra Juma ni vyema tukawaambia kwa uwazi na bila kupepesa macho kua Los Angeles Olympic 2028, hatutawaonea aibu, wala kuwafumbia macho ikiwa tutaendelea kua na ushiriki finyu na usio na mafanikio yanayoonekana. Watumie dhamana walizo nazo, na ushawishi walionao, Mtaka akiwa mkuu wa Mkoa na Bi Nasra akiwa kamishna msaidizi mstaafu wa Uhamiaji kufanya jambo litakalofanana na hadhi ya dhamana ya vyeo vyao. Wajumbe wa Mkutano Mkuu wametimiza wajibu wao, ni wakati na wao kutimiza wao. Tanzania inawatazama, safari imeanza sasa.

0 Comments