MWENDA KWAO SI MTUMWA

Katika Viwanja vya Sabasaba, timu ya Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ikiongozwa na Kamishna wa Uhifadhi Abdul-Razaq Badru tarehe 6 June, 2026 ilivifunika viwanja hivyo huku macho na masikio ya wananchi waliotembelea yakijielekeza kwenye Kampeni ya Ngorongoro inayojulikana kama Karibu Nyumbani.

Akizungumza na Waandishi wa Habari katika siku maalum ya Ngorongoro, Kamishna Badru amewaeleza kuwa umuhimu wa kampeni hiyo inatokana na historia kwa kuainisha wazi kuwa binadamu wa kale kutembea kwa miguu miwili historia yake alipatikana ndani ya hifadhi ya Ngorongoro.

Ameeleza kuwa ushahidi uliopo wa zaidi ya miaka milioni 3.6 unaonesha binadamu huyo aliweza kutembea na kufanya shughuli zake kwa kutumia zana za miaka hiyo, kuyatawala mazingira na kuishi bila shida yoyote.

Mhifadhi Mambokale wa Ngorongoro Ladislaus Kashaija akitoa maelezo kuhusu kwanini Ngorongoro inajivunia historia hiyo ameeleza kuwa inatokana na ushahidi wa wanazuoni duniani kote kuitaja Ngorongoro kama sehemu yenye ushahidi wa kutosha kuhusu historia ya binadamu.


Mchezaji wa timu ya soka ya Simba Shomari Kapombe amesema kuwa atakuwa chachu ya luwashawishi wanasoka wenzie kuitangaza Ngorongoro kuwa chanzo cha mpira wa miguu kwa kuwa historia ya binadamu kutembea kwa miguu miwili imeanzia hapo.

Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro imeshiriki tukio la siku ya Ngorongoro (Ngorongoro Day) katika viwanja vya sabasaba kwa kuhamasisha washiriki warudi Nyumbani Ngorongoro kwani mwenda kwao si mtumwa.

Post a Comment

0 Comments