JNHPP YAWAVUTIA WABUNGE; WASEMA NI FAHARI YA TAIFA NA MATUNDA YA KODI ZA WANANCHI


📌 Waipongeza Wizara ya Nishati na TANESCO kwa usimamizi mahiri wa mradi ulioimarisha upatikanaji wa umeme nchini.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa usimamizi mzuri wa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), ikieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 ambao umeimarisha upatikanaji wa umeme nchini na kuwa miongoni mwa miradi mikubwa barani Afrika.

Hayo yamebainishwa leo Juni 29, 2026 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu (Mb), wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika Mradi wa Kufua Umeme wa JNHPP uliopo Rufiji, mkoani Pwani, kwa lengo la kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo.

« Sisi kama Kamati tumeridhishwa na kazi kubwa iliyofanyika katika mradi huu hadi kukamilika kwake kwani mradi huu umeimarisha upatikanaji wa umeme nchini na unachangia takribani asilimia 45 ya umeme kwenye Gridi ya Taifa. Hivyo, nimpongeze Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza utekelezaji wa mradi huu wa kimkakati ambao umeleta suluhisho la kuimarisha upatikanaji wa umeme nchini, » amesema Mhe. Mgalu.

Aidha, Mhe. Mgalu amewashukuru wananchi kwa kulipa kodi ambazo zimepelekea mradi huo mkubwa kukamilika huku akisisitiza kuwa Kamati itaendelea kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa umeme wa uhakika wakati wote.

Amefafanua kuwa umeme unaozalishwa na JNHPP utaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme kupitia miradi mbalimbali ya usafirishaji wa umeme ikiwemo mradi wa Chalinze–Dodoma.

Vilevile, Mhe. Mgalu amesisitiza kuhusu kuimarisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme ili kuhakikisha umeme unaopatikana nchini unafika hadi ngazi ya vitongoji.

Post a Comment

0 Comments