Mwanahabari Mkongwe Irene Mark akichangia jambo katika mafunzo hayo ya siku moja.
Mwandishi wa Habari Mwandamizi Tamali Vullu akichangia hoja.
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limewataka waandishi wa habari nchini kujiunga na Mfumo wa Hifadhi ya Jamii wa Hiari (NSSF Hifadhi Scheme) ili kujenga usalama wa maisha yao baada ya kustaafu na kujikinga dhidi ya changamoto za kiuchumi na kiafya.
Wito huo umetolewa na Mweka Hazina wa TUCTA, James Kalanje, aliyemwakilisha Rais wa shirikisho hilo, Tumaini Nyamhokya, wakati wa ufunguzi wa semina maalum ya kuhamasisha wafanyakazi wa sekta ya habari kujiunga na NSSF Hiyari Scheme. Semina hiyo imeandaliwa na NSSF kwa wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA) jijini Dar es Salaam.
Kalanje amesema sekta ya habari ni nguzo muhimu ya demokrasia, uwazi na maendeleo ya taifa, lakini waandishi wengi, hususan wa sekta binafsi na wanaojitegemea, bado hawapo katika mifumo rasmi ya hifadhi ya jamii, hali inayowaweka katika hatari wanapokumbwa na uzee, maradhi au kushindwa kufanya kazi.
Amesema takwimu zisizo rasmi zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi wa vyombo vya habari nchini hawajajiunga na mifuko rasmi ya hifadhi ya jamii, jambo linalowalazimu baadhi yao kutegemea msaada wa ndugu na marafiki wanapokabiliwa na matatizo.
Kwa mujibu wa Kalanje, NSSF Hiyari Scheme ni fursa muhimu kwa wafanyakazi wa sekta binafsi na watu waliojiajiri kuweka akiba kulingana na uwezo wao, hatua inayowasaidia kujenga kipato cha uzeeni pamoja na kujikinga dhidi ya changamoto mbalimbali za maisha.
Ameongeza kuwa, mbali na akiba ya uzeeni, mpango huo unamwezesha mwanachama kupata huduma za bima ya afya, hivyo kunufaika na matibabu wakati wote wa uanachama wake.
Kalanje amewataka wanachama wa JOWUTA kutumia taaluma yao kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa hifadhi ya jamii, huku akisisitiza kuwa wanapaswa kuanza kwa kuwa mfano kwa kujiandikisha wenyewe katika mpango huo.
Pia amewataka waajiri wa vyombo vya habari kuweka mazingira yatakayowahamasisha wafanyakazi wao kujiunga na mifumo ya hifadhi ya jamii, akieleza kuwa wafanyakazi wenye uhakika wa maisha yao ya baadaye huzalisha kwa ufanisi zaidi na kufanya kazi kwa uaminifu.
Aidha, ameipongeza NSSF kwa kuendelea kutoa elimu kuhusu mpango huo kwa wanahabari, lakini akaishauri kupanua kampeni hiyo ili kuwafikia waandishi wa habari na makundi mengine ya sekta isiyo rasmi katika mikoa yote nchini.
Amesema hatua ya kuanza kutoa elimu kwa wanahabari wa Dar es Salaam na Pwani inapaswa kuendelezwa katika maeneo mengine ili Watanzania wengi zaidi wanufaike na mfumo wa hifadhi ya jamii wa hiari.
Akihitimisha hotuba yake, Kalanje amewahimiza waandishi wa habari kutochelewa kujiwekea msingi imara wa maisha yao ya baadaye kwa kujiunga na NSSF Hiyari Scheme, akisisitiza kuwa kuanza kuweka akiba mapema ni njia bora ya kujenga maisha yenye amani, heshima na uhakika baada ya kustaafu.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa NSSF Kinondoni, Gerald Mkonyi, amesema mfuko huo umejipanga kuhakikisha wanahabari wanapata elimu ya kutosha kuhusu hifadhi ya jamii ili waweze kufanya maamuzi sahihi yatakayowaletea usalama wa maisha wanapofikia umri wa kustaafu.





0 Comments