AIR TANZANIA YAZINDUA SAFARI ZA MOJA KWA MOJA DAR ES SALAAM–MUSCAT, OMAN


Muscat, Oman

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema uzinduzi wa safari za moja kwa moja za Shirika la Ndege la Air Tanzania kati ya Dar es Salaam na Muscat ni hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Sultanate ya Oman pamoja na kufungua fursa mpya za biashara, utalii, uwekezaji na usafirishaji.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa safari hizo jijini Muscat, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesema safari hizo zinajenga juu ya msingi wa uhusiano wa muda mrefu uliounganishwa na Bahari ya Hindi, ambapo kwa karne nyingi Watanzania na Waomani wamekuwa wakifanya biashara, kubadilishana maarifa, tamaduni na kujenga mahusiano ya kijamii na kifamilia.

"Uzinduzi wa leo si kufungua njia mpya ya ndege pekee, bali ni mwanzo wa sura mpya ya ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya mataifa yetu mawili," alisema Prof. Mbarawa

Ameeleza kuwa kuanza kwa safari za Air Tanzania kutatoa chaguo zaidi kwa wasafiri, kuongeza uwezo wa usafirishaji na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya safari za biashara na utalii kati ya Tanzania na Oman, huku ukikamilisha huduma ambazo zimekuwa zikitolewa na Oman Air.

Prof. Mbarawa amesema usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi kwani unaunganisha wafanyabiashara na masoko, watalii na vivutio, wawekezaji na fursa, pamoja na kuwaunganisha wananchi wa mataifa mbalimbali.

Amebainisha kuwa kupitia safari tatu za moja kwa moja kila wiki kati ya Dar es Salaam na Muscat, nchi hizo mbili zinatarajia kuongeza biashara, kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi, kurahisisha usafirishaji wa mizigo yenye thamani kubwa pamoja na kuimarisha mawasiliano ya familia na jamii zenye mahusiano ya kihistoria.

Aidha, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga kwa kuboresha miundombinu, kuimarisha usalama na ushindani wa sekta hiyo, pamoja na kuiwezesha Air Tanzania kupanua mtandao wa safari zake ndani na nje ya nchi.

Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa lengo la Serikali si kuongeza tu idadi ya safari za ndege, bali kuhakikisha kila njia mpya inaleta mchango chanya katika ukuaji wa uchumi wa taifa na kuimarisha uhusiano wa Tanzania na masoko ya kimataifa.

Akizungumzia ushirikiano wa Tanzania na Oman, Waziri Mbarawa amesema nchi hizo zina fursa kubwa za kushirikiana katika sekta za biashara, uwekezaji, usafiri wa anga na majini, utalii, kilimo, nishati, uvuvi na Uchumi wa Buluu.

Amewataka wafanyabiashara na wawekezaji wa Oman kutumia fursa zilizopo Tanzania kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali za uzalishaji na huduma, akieleza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Vilevile, amewahamasisha wananchi wa Oman kutembelea vivutio vya utalii vya Tanzania ikiwemo Mlima Kilimanjaro, Hifadhi za Taifa za Serengeti na Ngorongoro pamoja na visiwa vya Zanzibar, huku akiwakaribisha Watanzania kuitembelea Oman kujionea historia, utamaduni na fursa zake za kiuchumi.

Prof. Mbarawa amesema mafanikio ya njia hiyo mpya hayatapimwa kwa idadi ya safari au abiria pekee, bali kwa kiwango cha fursa za biashara, uwekezaji, utalii na maendeleo ya kiuchumi zitakazozalishwa kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Om🇴🇲 

Ametoa wito kwa Serikali, mashirika ya ndege, mamlaka za usafiri wa anga, waendeshaji wa viwanja vya ndege na sekta binafsi kushirikiana kuhakikisha njia hiyo inakuwa endelevu na yenye manufaa kwavizazi vya sasa na vijavyo.

Post a Comment

0 Comments