WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA MKUU WA MAJESHI WA MALAWI


Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), tarehe 20 Agosti 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Malawi, Jenerali George Jaffu, ambaye yupo nchini kwa ziara rasmi ya kikazi.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga, jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao wamejadili masuala mbalimbali yanayohusu ushirikiano wa kiulinzi na kijeshi kati ya Tanzania na Malawi. 

Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ameeleza kuridhishwa na uhusiano mzuri na wa muda mrefu uliopo kati ya Majeshi ya Tanzania na Malawi. 

Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha na kudumisha uhusiano huo wa kihistoria kwa manufaa ya nchi na wananchi wa mataifa hayo mawili. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Malawi, Jenerali George Jaffu, ametoa shukrani kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msaada mbalimbali ambao umekuwa ukitolewa kwa Malawi kupitia Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). 

Jenerali Jaffu ametoa shukrani hizo akirejea, miongoni mwa misaada hiyo, msaada wa chakula uliotolewa na Serikali ya Tanzania na kusafirishwa hadi Malawi kupitia JWTZ, akieleza kuwa hatua hiyo imeendelea kudhihirisha mshikamano na undugu wa muda mrefuuliopo kati ya Tanzania na Malawi. 

Jeshi la Wananchi wa Tanzania na Jeshi la Ulinzi la Malawi yamekuwa yakishirikiana kwa karibu katika masuala mbalimbali ya kijeshi, ikiwemo mafunzo, kubadilishana uzoefu pamoja na kufanya mazoezi ya pamoja, hatua inayochangia kuimarisha uwezo na uhusiano wa kiutendaji baina ya Majeshi hayo. 

Katika ziara yake nchini Tanzania, Jenerali George Jaffu anatarajiwa kutembelea maeneo mbalimbali, ikiwemo mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, pamoja na maeneo ya utalii, kwa lengo la kujionea na kufahamu zaidi vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini.

Ziara hiyo inaendelea kudhihirisha uhusiano wa karibu, urafiki na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Tanzania na Malawi, hususan katika masuala ya ulinzi na usalama.

Post a Comment

0 Comments