Na. Mwandishi Wetu - Mwanza
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi ashauri kikundi cha Paza Sauti cha Watu Wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (WAVIU) kutumia mitandao ya kijamii kutangaza na kuuza bidhaa zao ili kuweza kufikia wateja wengi zaidi huku akiwapongeza kwa juhudi na umoja wao katika shughuli zao za uzalishaji.
Ametoa ushauri huo alipotembelea kikundi cha Paza Sauti cha wajasiliamali wanaoishi na VVU katika ziara yake ya ufatiliaji utekelezaji wa afua za VVU na UKIMWI katika Wilaya ya Nyamagana, Jijini Mwanza.
“Nikiingia kwenye simu yangu sioni kikundi cha Paza Sauti msibanwe na soko la machoni nendeni duniani kupitia mitandao ya kijamii, anzisheni akaunti ya Instagram muweze kuwafikia hata watu walipo nchi za nje" alisema Dkt. Yonazi.
Dkt. Yonazi alitembelea Kikundi cha Peace and Love kinachojishughulisha na kilimo cha nyanya na matikiti, kinachosimamiwa na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kupitia Mradi wa DREAMS, unaoratibiwa na TACAIDS kwa kushirikiana na ICAP, Mradi huo unalenga kuwawezesha wanawake na vijana balehe kiuchumi na kijamii ili kupunguza vishawishi vinavyoweza kupelekea maambukizi mapya kwa kundi hili.
Kwa hatua nyingine Dkt.Yonazi amepongeza Jiji la Mwanza kwa kuweza kufanikiwa kufikia lengo la kitaifa la 95-95-95 kwa kiwango cha juu na kuongeza ushirikiano na wadau wakiwemo viongozi wa dini katika mwitikio wa VVU na UKIMWI nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji waTume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Adam Mrisho alisisitiza kuwa TACAIDS itaendelea kuwekeza katika uwezeshaji wa vijana kiuchumi kama sehemu ya juhudi za kuwaondoa katika mazingira ya changamoto na vishawishi vinavyoweza kuongeza hatari ya maambukizi mapya ya VVU.
“hongereni kwa juhudi na kazi mnazozifanya, hili ni eneo ambalo Tume tumezingatia sana ili kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi”walisema
Naye, Katibu wa Baraza la Watu Wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI Wilaya ya Nyamagana Joseph Kiharate ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu kwa kuwezesha WAVIU kupata dawa katika hospitali zote na kushukuru huduma zinatolewa kwani zinazingatia ubora na weledi kwa kila siku katika juma.
“tunashukuru tunapata dawa katika hospitali zote na huduma zinatolewa siku saba za wiki kupitia nyie afya zetu zinaimarika," alisema Joseph.




0 Comments