TBN YAAHIDI KUWA BALOZI MWEMA WA PSSSF

 

DAR ES SALAAM

Mtandao wa Wanablogu Tanzania (Tanzania Bloggers Network—TBN) umetangaza dhamira yake ya kuendelea kushirikiana na taasisi za umma na binafsi katika kusambaza maudhui bora yanayoelimisha jamii na kuitangaza vyema Tanzania kupitia majukwaa ya kidijitali.

Akizungumza katika mkutano baina ya viongozi wa TBN na ujumbe kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), uliofanyika katika Makao Makuu ya TBN, Kijitonyama jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa TBN, Beda Msimbe, alisema wakati umefika kwa taarifa chanya za maendeleo kupewa nafasi kubwa zaidi katika ulimwengu wa kidijitali.

Alisema umuhimu wa hatua hiyo umeongezeka katika kipindi hiki ambacho teknolojia ya akili unde imewezesha taarifa kutafutwa, kupatikana na kusambazwa kwa kasi kubwa kuliko wakati mwingine wowote.

“Ni jambo la kusikitisha kuona taarifa zinazoongoza katika mifumo ya habari za kidijitali na kusambaa duniani kote kuhusu Tanzania mara nyingi ni zile zinazotokana na matukio ya udaku mitandaoni, badala ya habari muhimu za maendeleo,” alisema Msimbe.

Akitoa mfano, alisema wakati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuwa akizindua Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere, wenye manufaa makubwa kwa Taifa, baadhi ya taarifa zilizovuma zaidi mitandaoni kutoka Tanzania hazikuhusu umuhimu wa mradi huo, bali maisha binafsi ya nyota wa filamu na muziki.

Msimbe alisema hali hiyo inaonesha umuhimu wa taasisi, vyombo vya habari na wadau wengine kushirikiana kuhakikisha mafanikio ya maendeleo ya Taifa yanapewa uzito unaostahili katika majukwaa ya kidijitali.

“TBN ipo tayari kushirikiana na taasisi mbalimbali kuongeza wingi wa taarifa chanya katika mifumo ya habari za kidijitali. Tunapaswa kuhakikisha Tanzania haitambuliki kwa habari zinazohusu maisha binafsi ya watu pekee, bali pia kwa mafanikio yake makubwa ya kiuchumi na kijamii,” alisema.

Msimbe alieleza kufurahishwa na dhamira ya PSSSF ya kushirikiana na TBN katika kupanua utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu hifadhi ya jamii, mifumo ya pensheni na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo.

Alisema TBN ina wanachama zaidi ya 200 waliopo nchini na nje ya nchi, wenye uwezo wa kuwafikia wananchi wengi kupitia majukwaa mbalimbali ya kidijitali.

“Tupo tayari kutumia uwezo, uzoefu na wigo mpana wa majukwaa ya wanachama wetu kutoa elimu sahihi kuhusu shughuli, huduma, uwekezaji na mifumo mbalimbali inayosimamiwa na PSSSF,” alisema Msimbe.

Kwa upande wake, Mdhamini wa TBN, Issa Michuzi, alisema mtandao huo una historia kubwa katika maendeleo ya habari za kidijitali nchini na unajivunia kuwa na wanachama wenye weledi, uzoefu na uwezo mkubwa wa kuwafikia wananchi.

Michuzi alisema TBN ilianzishwa kwa dhamira ya kuhakikisha Tanzania inajenga taswira nzuri katika medani za kidijitali kwa kusambaza taarifa sahihi, zenye manufaa na zinazochochea maendeleo ya Taifa.

“TBN ipo tayari kushirikiana na PSSSF kuhakikisha elimu ya hifadhi ya jamii inawafikia wananchi kwa lugha nyepesi, sahihi na inayoeleweka kupitia majukwaa ya kidijitali,” alisema Michuzi.

Naye Katibu wa TBN, Rahel Pallangyo, alisema mtandao huo upo tayari kutumia waandishi wake mahiri pamoja na majukwaa ya wanachama wake kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na zenye kuaminika.

Alisema taarifa hizo zitawawezesha wananchi kuelewa vyema haki na wajibu wao pamoja na fursa zinazopatikana kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii.

Pallangyo alisema ushirikiano baina ya TBN na PSSSF unaweza kuwa daraja muhimu la kuiunganisha taasisi hiyo na wananchi, hususan katika kipindi hiki ambacho majukwaa ya kidijitali yamekuwa miongoni mwa vyanzo vikuu vya habari, elimu na maarifa.

Akizungumza kwa niaba ya PSSSF, Mkuu wa Msafara, Abdul Njaidi, alisema ziara hiyo ilikuwa sehemu ya jitihada za mfuko kujenga uhusiano wa karibu na wadau wa sekta ya habari na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii.

Njaidi aliwahakikishia viongozi wa TBN kuwa maombi, mapendekezo na hoja zote zilizowasilishwa katika mkutano huo zitafanyiwa kazi.

Alisema dhamira ya PSSSF ni kuhakikisha wananchi wanapata uelewa mpana na sahihi kuhusu masuala ya pensheni na hifadhi ya jamii pamoja na uwekezaji unaofanywa na mfuko huo kwa manufaa ya wanachama na Taifa kwa ujumla.

Ujumbe wa PSSSF uliongozwa na Abdul Njaidi na kuwajumuisha Regina Kumba, Grayson Mgunda na Doreen Lyimo.

Kwa upande wa TBN, mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti Beda Msimbe, Katibu Rahel Pallangyo, mtaalamu wa mawasiliano Cathbert Kajuna na Mdhamini Issa Michuzi.

Post a Comment

0 Comments