*Tanzania Yaingia Ramani ya Dunia kama Mzalishaji wa Ferro-Niobium, Namba Tatu Baada ya Canada na Brazil*
*Barrick Gold Yaanza Utafiti wa Kina wa Dhahabu Nzega, Kahama*
*Ununuzi wa Dhahabu wa Tani 17 Tanzania kuingia 10 Bora Barani Afrika*
Na Wizara ya Madini, Dodoma
Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amesema kuwa Serikali ya Tanzania inatarajia kusaini mikataba mikubwa na kampuni za madini mapema mwezi Februari 2026, kwa ajili ya uchimbaji wa madini mbalimbali, ukiwemo wa niobium katika bonde la Songwe Panda Hill, Mkoa wa Mbeya.
Amesema hayo Januari 26, 2026, jijini Dodoma, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa ahadi za Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alizozitoa wakati wa kampeni zake na pindi akihutubia Bunge la 13 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wakati akiwaapisha Mawaziri.
“Mbali na uchimbaji, mradi huo utajengwa pamoja na kiwanda cha kusafisha na kuongeza thamani cha niobium, kitakachozalisha Ferro-Niobium,” amesema Mavunde na kuongeza kwamba, hatua hiyo itaiweka Tanzania kwenye nafasi ya nne kati ya wazalishaji wakuu duniani, nyuma ya Canada na Brazil.
Mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Shilingi Trilioni 1 na utakuwa kichocheo kikuu cha ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa ajira.
Aidha, Waziri amebainisha kuwa kampuni ya kimataifa ya madini ya dhahabu, Barrick Gold, iko tayari kuanza utafiti wa kina wa madini Wilayani Nzega, Mkoa wa Tabora na Kahama Shinyanga na kusema, “utafiti huu wa kina ni hatua ya msingi kuelekea uanzishwaji wa mgodi mpya mkubwa wa dhahabu katika mkoa huo,".
Akizungumzia hali ya utafiti wa jiolojia nchini, amesema kuwa hadi sasa, asilimia 97 ya nchi imefanyiwa utafiti wa msingi wa jiolojia, asilimia 100 ya utafiti wa kimagnetiki, na asilimia 24 ya utafiti wa jiokemia. “Lengo la Serikali ni kuongeza wigo wa utafiti huu hadi kufikia asilimia 50 ifikapo mwaka 2030, kwa kufuata Dira yetu: ‘Madini ni Maisha na Utajiri’,” ameongeza.
Kuhusu ununuzi wa madini ya dhahabu unaoendelea na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Waziri Mavunde amebainisha kuwa katika kipindi cha miezi 14 tangu Oktoba 2024, BoT imenunua na kuhifadhi tani 17 za dhahabu kama amana ya taifa. Kiasi ambacho kinaiweka Tanzania kwenye nafasi ya 10 kati ya nchi zenye hifadhi kubwa za dhahabu barani Afrika, kikiipita Msumbiji (tani 6.89) na kukaribia nchi zinazoongoza kama Algeria (tani 174).
Kuhusu jinsi Sekta ya Madini inavyochangia agenda ya Mhe. Rais ya kukuza matumizi ya nishati safi, Waziri amesema kuwa kupitia Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kiwanda kipya cha kuzalisha mkaa mbadala wa ‘Rafiki Briquettes’ kutokana na makaa ya mawe kinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni mkoani Tabora “Briquettes hizi zitasaidia katika ukaushaji wa zao la tumbaku na kupunguza matumizi ya kuni,” amesema.
Pia, ametaja juhudi za Serikali kurejesha hadhi ya Tanzania katika soko la madini la ndani na la kimataifa. “Ndani ya siku 100 hizi, kupitia ushirikiano kati ya Tume ya Madini na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), tumeweza kufanikisha mnada wa kwanza wa madini ya vito jijini Arusha, na kuweka msingi wa soko la ndani lenye nguvu,” ameongeza Mhe. Mavunde.
*Dira ya 2030: Madini ni Maisha na Utajiri*


0 Comments