Na Mwandishi Wetu, Ngorongoro.
Tofauti na vijana wa mjini hasa wa Dar es Salaam ambao wengi wao hutahiriwa wakiwa wadogo hospitalini tena kwa ganzi, tohara kwa vijana wa kimasai hufanyika wakiwa mabarobaro na mashabaro na tena bila ganzi na hivyo kusikia maumivu makali ya kitendo hicho.
Katika kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imeungana naye kwa kupanda miti aina ya Olorien katika kijiji cha Oloirobi Wilayani Ngorongoro.
Miti hiyo hukatwa na hutumika mara baada ya vijana wa kimasai kufanyiwa Jando/kutahiriwa, kijana akishatahiriwa miti huo huwekwa mlangoni wa nyumba yenye kijana aliyetahiriwa kisha akina mama huzunguka ulipowekwa mti husika huku wakiimba kwa furaha na vigelegele kuashiria kwamba zoezi la tohara limefanyika na kukamilika.
Kwa mujibu wa imani ya kabila hilo nyimbo za shangwe na faraja zinazoimbwa na kina mama kwa kuzunguka mti huo ukiwa kwenye nyumba humfanya kijana kuwa na faraja kutofikiria maumivu aliyoyapata wakati wa tohara.
Tohara katika kabila la wamasai inahusisha mafundisho yote ya msingi kwa mwanaume ikiwa ni pamoja na kuwafanya wawe majasiri na shujaa wanaoweza kukabiliana na changamoto zozote za kimaisha tofauti na vijana wanaozaliwa mjini maarufu kama vijana wa elfu mbili (2000) ambao wengi wao maumivu ya jando hawayafahamu kutokana na kutahiriwa wakiwa wadogo tena wengi wao wakifanyiwa tohara hospitali.Akizungumza mara baada ya zoezi hilo la upandaji wa miti Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayesimamia Idara ya Maendeleo ya Jamii Gloria Bideberi amesema kuwa mamlaka itaendelea kuithamini miti hiyo na kushirikiana na jamii ya kabila hilo kuhakikisha miti hiyo haitoweki
Kiongozi wa kimila wa kata ya Ngorongoro bwana Sembeta Ngoidiko amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kusherehekea siku yake ya kuzaliwa kwa kupanda miti na kusema na wananchi wa kijiji cha Oloirobi kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro wameamua kupanda miti hiyo pamoja na miti mingine inayotumika kama miti dawa ili kuendelea kudumisha uhifadhi,mila na desturi.








0 Comments