Tabora
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kusisitiza umuhimu wa usimamizi shirikishi wa misitu ya Miombo ili kukabiliana na uharibifu wa mazingira na upotevu wa bioanuwai.
Hayo yamejitokeza katika kikao cha pili cha Kamati ya Ushauri ya Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo ya Nyanda Kame (Drylands Sustainable Landscape Impact Program – DSL-IP) kilichofanyika Machi 4, 2025, katika ukumbi wa JM Hotel, Tabora.
Akisoma hotuba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Bernard Marcelline, alisema kuwa mradi huo ni sehemu ya juhudi za kitaifa na kimataifa za kulinda mazingira kwa kutumia mbinu shirikishi za usimamizi wa mandhari.
"Mradi huu unatekelezwa kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) na unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF). Utekelezaji wake unahusisha mikoa ya Tabora na Katavi, ambapo zaidi ya shilingi bilioni 2.2 tayari zimepokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza,” alisema Marcelline.
Ameeleza kuwa kikao hicho cha Kamati ya Ushauri kina jukumu la kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia malengo yaliyopangwa. Pia amesisitiza kuwa juhudi za uhifadhi zinapaswa kuhusisha wadau wote, akiwemo wananchi wa maeneo husika, ili kuhakikisha misitu ya Miombo inatunzwa kwa faida ya kizazi cha sasa na kijacho.
Mwakilishi Mkazi wa FAO nchini Tanzania, Dkt. Nyabenyi Tipo, akizungumza katika kikao hicho, alisisitiza kuwa mradi huu ni sehemu ya mpango mpana wa usimamizi endelevu wa mazingira katika nchi 11, zikiwemo Angola, Botswana, Malawi, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe, Tanzania, Kenya, Burkina Faso, Mongolia na Kazakhstan.
"Kila mwaka, takriban hekta milioni 7.3 za misitu hupotea duniani, huku Tanzania ikipoteza zaidi ya hekta 469,420. Kupitia mpango huu, FAO imejidhatiti kusaidia juhudi za kuhifadhi mazingira kwa kutumia mbinu za usimamizi wa mandhari endelevu,"_ alisema Dkt. Tipo.
Alibainisha kuwa Tanzania ina nafasi muhimu katika utekelezaji wa programu hiyo, hususan katika kukuza uzalishaji endelevu wa ufugaji nyuki. FAO tayari imetoa jumla ya dola za Kimarekani 883,640, ambazo ni asilimia 13 ya jumla ya dola milioni 6.8 zilizopangwa kutolewa kati ya 2023 na 2027.
"Natoa wito kwa wadau wote kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi ili kuhakikisha unaleta matokeo chanya kwa wakati,” aliongeza.
Aidha, Dkt. Tipo aliipongeza Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa utekelezaji wa mradi huo chini ya makubaliano ya ushirikiano wa utekelezaji (Operational Partners Agreement – OPA).
"Mradi huu unaendana na Mkakati wa Kimkakati wa FAO 2022-2031 unaolenga kusaidia Ajenda ya Maendeleo ya 2030. Katika mwaka huu wa 80 wa FAO, tuna fursa ya kushirikiana kuleta mabadiliko makubwa katika mifumo ya uzalishaji wa chakula na uhifadhi wa mazingira,” alisisitiza
Dkt. Tipo alihitimisha hotuba yake kwa kuwashukuru Prof. Dos Santos Silayo, Kitengo cha Usimamizi wa Mradi (PMU) na wadau wote wanaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo, akisema anatarajia kikao hicho kitakuwa na mafanikio makubwa katika kusukuma mbele juhudi za uhifadhi wa mazingira.


0 Comments