Na Kassim Nyaki, NCAA.
Wataalamu
wa UNESCO waliowasili nchini mapema wiki hii kwa ajili ya uthibitishaji
upya (Revalidation) wa Hifadhi ya kijiolojia ya "Ngorongoro Lengai
UNESCO Global Geopark" na kutembelea maeneo mbalimbali ndani na nje ya
hifadhi ya Ngorongoro wamehitimisha ziara hiyo leo tarehe 25 Julai, 2024
kwa kufanya kikao cha mwisho (exit meeting) kilichojumuisha menejimenti
ya NCAA, mwakilishi wa UNESCO na NATCOM Tanzania pamoja na wawakilishi
wa Wilaya za Karatu na Monduli mkoani Arusha.
Wakati
wa ziara yao ndani na nje ya hifadhi hiyo ujumbe huo ulitembelea eneo
linalojengwa Makumbusho ya Hifadhi ya Kijiolojia ya Ngorongoro-Lengai
UNESCO Global Geopark, eneo la nyayo za Laetoli, Makumbusho ya Olduvai,
bonde la Olduvai, mchanga unaohama, jamii za makabila ya wairaqw,
wahadzabe na wadatoga zinazoishi pembezoni mwa ziwa Eyasi katika wilaya
ya Karatu.
Ujumbe huo pia
umetembelea shule ya msingi za Tumaini Junior Pre and Primary School na
shule ya Father Lieberman Pre and Primary School zilizoko Karatu,
kutembelea na kuona shughuli za uwindaji, uhunzi, urithi wa utamaduni na
utunzaji wa mazingira zinazofanywa na wanafunzi na makabila
yanayozunguka hifadhi ya Ngorongoro ili kuona jinsi hifadhi
inavyoshirikisha jamii kusaidia kuhifadhi urithi wa utamaduni wao na
mazingira yanayowazunguka.
Aidha,
wataalam hao ambao ni wabobezi katika eneo la utalii wa Jiolojia na
akiolojia wametembelea Kreta ya Ngorongoro kuona alama mbalimbali za
jiopaki pamoja na kutembelea eneo la Laetoli kuangalia tabaka mbalimbali
zilizotunza historia ya kidunia kuhusu wanyama na binadamu wa kale
duniani walioishi takribani miaka milioni 3.6 iliyopita na kuona
jitihada za Serikali kupitia NCAA katika uhifadhi wa urithi huo.
Kamishna
wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Elirehema Doriye akiwaaga wataalam hao
amewahakikishia kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuhifadhi, kulinda,
kutangaza na kufuata masharti na miongozo ya UNESCO katika kulinda hadhi
ya eneo hilo ili kuendelea kuwa Hifadhi ya Kijiolojia inayotambulika
kama “Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark” ambapo Tanzania ni nchi
ya pili Afrika kuwa na hadhi hiyo baada ya nchi ya Moroco.
Maeneo
yenye hadhi za Jiolojia (Geopark) za UNESCO zinakaguliwa kwa kina kila
baada ya miaka minne kwa ajili ya kupima na kuona ufanisi na ubora wao
kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maeneo hayo kwa kufuata
vigezo vilivyoainishwa na UNESCO.
0 Comments