Unaweza kusema dili limetiki kufuatia klabu ya Simba ya Jijini Dar es Salaam kuchagua kivutio namba moja cha utalii barani Africa kufanya uzinduzi wa wiki ya simba na jezi mpya ya mnyama kwa mwaka 2026.
Uzinduzi uliofanyika leo tarehe 1 Agosti, 2026 eneo la Ngoitoktok katika kasoko ya Ngorongoro ulipambwa na upepo mwanana unaotokana na mawimbi kutoka bwawa la Ngoitoktok likipambwa na Viboko wanaogelea huku ulinzi ukiimarishwa na familia za Simba waliosheheni kreta ya Ngorongoro.
Akizungumzia tukio hilo la kihistoria lililojumuisha uzinduzi wa logo ya miaka 90 ya Simba ulihudhuriwa na menejimenti ya Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro iliyoongozwa na Naibu Kamishna huduma za Shirika Aidan Makala na mashabiki zaidi ya 300 kutoka ndani na nje ya Nchi.
“Tukio hili ni matokeo chanya kati ya ushirikiano wa Klabu ya Simba na hifadhi ya Ngorongoro, tumetangaza utalii wa ndani, wanasimba wamerudi nyumbani lakini kubwa zaidi ni kuchagiza utalii wa michezo kuelekea mashindano ya AFCON ya mwaka 2027 yatakayofanyika hapa Nchini” Naibu Kamishna Aidan Makala.
Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu ya Simba Ahmed Ally amebainisha kuwa Ngorongoro ni zaidi ya hifadhi, ina vivutio vingi vya utalii ambapo asili, urithi wa utamaduni na malikale vinaishi pamoja, hivyo Simba kufanya uzinduzi huo ndani ya hifadhi ni kurudisha mashabiki nyumbani na kuwadhihirishia kuwa ndoto, maono na hisia zao zinakutana na uhalisia uliopo Ngorongoro.


0 Comments