WAZIRI NAPE ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KIFO CHA SARA DUMBA

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye ametuma salamu za rambirambi kwa wanahabari wote kufuatia kifo cha ghafla cha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Njombe na Mtangazaji Mwandamizi wa zamani wa Redio Tanzania (RTD), Dar es salaam Marehemu Sara Dumba.

“Pokeeni salamu za rambirambi zangu za dhati kwa kuondokewa na Mwanahabari mahiri Bi. Sara Dumba aliyekuwa mfano wa kuigwa” amesema Mhe. Nape.

“Mbali na utangazaji wake mahiri, Bi. Sara Dumba alikuwa mzalendo wa kweli aliyetumikia tasnia hii ya Habari na Serikali kwa uadilifu na upendo wa kweli, tutamkumbuka na tutaukosa mchango wake.

Ni wajibu wetu kumuombea mapumziko mema kwa mwenyezi Mungu na kumshukuru kwa mchango wake alioutoa kwa moyo wa dhati”.

“Hakika Sara tutamkumbuka, nawapa pole wananchi wote wa wilaya ya Njombe kwa kuondokewa na kiongozi wao mpendwa mwenzao”,ameongeza Waziri Nape.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Profesa Elisante Ole Gabriel naye ametuma salamu hizo “Salaam ziwafikie familia, ndugu jamaa na marafiki walioguswa na msiba huu ambao unawagusa sana, naelewa machungu waliyonayo na huzuni, hata hivyo kwa pamoja ni wakati wa kuzidi kumuombea Marehemu katika safari yake ya mwisho”,amesema Profesa Elisante na kuwatakia moyo wa subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.

Baadhi ya wafanyakazi wenzake waliowahi kufanya kazi pamoja naye ambao ni Aloisia Maneno amesema Bi. Sara alikuwa mwalimu wake katika masuala ya utangazaji kwa kuwa ndiye aliyemfundisha jinsi ya kuandaa kipindi cha watoto cha Cheichei Shangazi.

Abdul Ngarawa amesema kuwa Bi. Sara alikuwa mchapakazi hodari, mtu mwenye kipaji cha utangazaji, mcheshi, mtu mwenye ushirikiano na wafanyakazi wenzake na jasiri asiyeogopa kusema ukweli hata kwa wakuu wake wa kazi pale ambapo kazi hazikufanyika vizuri.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Hajjat Halima Kihemba akizungumzia uhusiano wake na marehemu amesema kwamba yeye alianza kazi RTD mwaka 1971 ambapo Bi. Sara alimkuta tayari akiwa kazini kati ya mwaka 1974, hivyo walifanya naye kazi pamoja kwenye Idhaa ya Kiingereza ya (External Services) marehemu akiwa msaidizi wake.

“Alikuwa ni mtu mwenye mchango mkubwa na yuko tayari kufanya kazi wakati wote unapomwihitaji usiku na mchana, mshauri hususan kwa watoto wa kike kuacha kujidharau na kuona kwamba hawezi kufanya kazi ya taaluma ya habari na mtu aliyependa maendeleo.

Kwa upande wake, Bakari Msulwa ambaye ni Mkuu wa Kanda ya Kati Dodoma - TBC akimzungumzia Bi.Sara Dumba amesema kuwa alihamishiwa mkoani Morogoro mwaka 1990 akiwa mwakilishi wa RTD na baade Mkuu wa Kanda ya Kati Dodoma hadi alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilindi mwaka 2006 .Ameongeza kwamba ni mama aliyekuwa mstari wa mbele katika kutetea haki za wanawake, aliandaa vipindi mbalimbali vya biashara na alikuwa yuko tayari kuambiwa ukweli.

" Kwa kweli Bi. Sara alijenga historia nzuri katika tasnia ya masuala ya habari na utumishi wa umma akiwa katika ngazi ya ukuu wa wilaya, hivi karibuni nilionana naye mkoani Tabora miezi miwili iliyopita alikuwa na mtazamo wa kuwaunganisha wafanyakazi wa RTD ili waweze kuwa na umoja utakaoweza kutupatia nafasi ya kusaidiana kwenye masuala mbalimbali,” Amesema Msulwa.

Msulwa amebainisha kuwa Bi. Sara alisema hayo baada ya kubaini kwamba hakuna historia ya wafanyakzi wa RTD.

Hivyo ameacha changamoto kwa hao kuacha historia zao ili ziweze kuwa na manufaa kwa watu wengine. Bi. Sara amefariki dunia tarehe 21 Machi, mwaka 2016 Wilayani Njombe, baada kuugua ghafla. Alizaliwa Oktoba 19, 1956. Bi. Sara alianza kazi katika Radio ya Taifa, Radio Tanzania Dar-es-Salaam (RTD) na baadaye Shirika la Utangazaji Taifa (TUT) sasa TBC.

Marehemu Sara Dumba kabla ya kuteuliwa kuwa mkuu wa Wilaya mwaka 2006 alivuma katika kipindi cha Majira(yaani habari za hapo kwa hapo) na vipindi vingine vingi. Kwa mujibu wa taarifa za Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe Jackson Saikadau amesema mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa kesho Machi 24, mwaka huu jijini Dares Salaam na kuzikwa nyumbani kwake eneo la Mbutu Mwembe Mdogo, Kigamboni.

Mwenyezi Mungu ailaze Roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.

IMETOLEWA NA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO 23, MACHI, 2016.

Post a Comment

0 Comments