Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu , Sheikh Issa Ponda akisoma gazeti la Tanzania Daima nyumbani kwake Mabibo Jijini Dar es Salaam jana,(Picha na Francis Dande).
NA KHADIJA KALILI
AFYA ya Katibu wa Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu, Sheikh Issa Ponda, inaendelea vizuri baada ya kufanyiwa
upasuaji wa henia Desemba 6, mwaka huu.
Hivi sasa kiongozi huyo mwenye
wafuasi wengi waamini wa Kiislamu yupo mapumziko nyumbani kwake Mabibo jijini
Dar es Salaam.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumatano iliyomtembelea nyumbani
kwake, Sheikh Ponda alikiri kufanyiwa upasuaji huo kwenye Hospitali ya Tabata
General na kubainisha kwamba ugonjwa huo ulimuanza miezi sita baada ya kuswekwa
mahabusu katika Gereza la Segerea jijini humo.
“Ni wiki mbili zilizopita ndiyo
nimefanyiwa upasuaji huu… nimeshatolewa nyuzi na hivi sasa nauguza kidonda tu
kama unavyoniona.
“Nilianza kupata maumivu
makali nikiwa Gereza la Segerea, zipo taratibu za kufuatwa ili mfungwa au
mahabusu apelekwe hospitalini. Nilizifuata lakini nikagundua kulikuwa na
urasimu ndiyo maana sikupelekwa hospitali,” alisema Sheikh Ponda aliyewahi
kuitikisa serikali kutokana na misimamo yake ya kutetea Uislamu.
Baada ya kuachiwa huru na
Mahakama ya Mkoa wa Morogoro Novemba 30, mwaka huu, siku mbili baadaye Sheikh
Ponda alikwenda hospitali ambapo daktari wake alimshauri afanyiwe upasuaji ili
kumnusuru na maumivu yaliyosababishwa na henia hiyo.
“Daktari alisema nimecheleweshwa
sana kuanza tiba lakini namshukuru Mwenyezi Mungu upasuaji ulikwenda vizuri na nimekwisha
kuondolewa nyuzi… hapa natibu mshono tu,” alisema.
Alisema akiwa gerezani
hakuchoka kuomba ruhusa ya kwenda hospitali kwa matibabu lakini jitihada zake
hazikufanikiwa.
“Hata nilipohamishiwa katika Gereza
la Morogoro na baadaye Ukonga, kote huko nilikuwa nawasiliana na viongozi wa
gereza nikiwaomba wanipeleke hospitali, sikufanikiwa hadi nilipoachiwa huru,”
alisema Ponda.
Aliishauri serikali kuwajali mahabusu
na wafungwa kwa kuwapa huduma bora hasa matibabu kwa kuwa ni haki yao.
“Huko magereza hali ni mbaya,
watu wanaumwa na kwa sababu hawapati tiba haraka ugonjwa unakua na kama
unaambukizwa, watu wanaambukizana, hakuna anayewajali kwa matibabu,”
alisisitiza.
0 Comments