TAMKO KATIKA UZINDUZI WA KAMPENI YA MAJI KIPINDI CHA UCHAGUZI

TGNP Mtandao kwa kushirikiana na Mtandao wa Maji na wanawake nchini umeandaa warsha ya siku moja pamoja na kongamano la maji yanayolenga kuimarisha uelewa wa wanaharakati na wananchi kwa ujumla juu ya masuala ya maji na hivyo kuendelea kudai haki ya maji kwa wananchi wote. Hayo yanafanyika kwa kipindi hiki kutumia uchaguzi mkuu kama fursa ya kuendeleza ajenda ya kudai haki ya upatikanaji wa huduma ya maji kwa jamii ya kitanzania, kwa makundi yote yaliyoko mijini na vijijini.

SIKU YA KWANZA 18/08/2015

Hii ilikuwa siku mahsusi kwaajili ya warsha ambapo washiriki kutoka Mtandao wa maji na wanawake nchini hususani kutoka mikoa ya Pwani, Dar es salaam, Kilimanjaro,……….wwalipata nafasi ya kujifunza, kubadilishana uzoefu, kujadilianan na kuweka mikakati madhubuti ya kubeba ajenda ya maji hasa wakati huu wa uchaguzi. Washiriki hao ni pamoja na vopngozi wa dini, wanaharakati ngazi ya jamii na taifa, waandishi wa habari pamoja na asasi za kiraia zinazopigania haki za binadamu.

SIKU YA PILI 19/08/2015

Siku hii ni ya mjadala wa wazi, kushirikisha uma kwa upana na kuutabanaisha umma juu ya tatizo la maji na umuhimu wa kudai haki yao ya msingi wa huduma ya maji. Badala ya kujadili tu siasa, hii itakuwa nafasi mahsusi ya kuhusisha uchaguzi na matatizo yanayowakabili wananchi wengi. Siku hii ni mahsusi katika kuzindua kampeni yetu ya maji “Tua Ndoo kichwani, Kura yangu Mustakabali Wangu”. Hii ni kampeni inayolenga kutumia fursa ya uchaguzi katika kuchochea mabadiliko katika sekta ya maji na hivyo kumwondolea mwanamke adha na mzigo wa maji pamoja na mizigo mingine ambatani inayotokana na mifumo kandamizi ya utoaji huduma za kijamii.

HALI YA UPATIKANAJI WA HUDUMA YA MAJI NCHINI

ž  Tanzania ni nchi kubwa katika Afrika Mashariki, yenye zaidi yawatu milioni 45.
ž  Licha ya uwepo wa vyanzo vingi vya maji nchni, zaidi ya watanzania milioni 14 hawapati maji safi na salama. Hii inamaanisha kuwa watu hawa wanalazimika kunywa maji machafu kutoka katika vyanzo visivyokuwa salama. Inadi kubwa ya watu hawa huishi maeneo ya vijijini.
ž  Zaidi ya watoto 7,000 hufariki kila mwaka kwa sababu ya ugonjwa wa kuhara unaoletwa na mazingira machafu na ukosekanaji wa huduma ya maji
ž  Karibu watu milioni 27 wanaishi katika mazingira yasiyo safi

Kwa ujumla makundi yanayoathirika zaidi kutokana na upungufu mkubwa wa maji ni pamoja na wanawake, wanafunzi hasa wa kike, watoto, wazee na walemavu. Hivyo, kwa kupitia kampeni yetu ya maji “Tua ndoo kichwani, kura yangu mustakabali wangu” tunaamini kuwa imefika wakati wa kumtua mwanamke ndoo ya maji kichwani pamoja na kumtua mizigo mingine anayobebeshwa mwanamke katika jamii na nchi yetu hivyo kuleta usawa wa kijinsia. Tunaamini tatizo la maji likiondolewa linaweza kuondoa matatizo mengine yanayoikumba jamii ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia ambao unaambatana na matatozo ya maji, mimba za utotoni, utoro mashuleni hasa kwa wanafunzi wa kike ambao katika maeneo mengi hushindwa kuhudhuria masomo kutokana na ukosefu wa huduma ya maji hasa wakati wakiwa katika siku zao za mwezi, pamoja na utatuzi wa kero za upatikanaji wa maji katika taasisi za afya kama vile zahanati, vituo vya afya na hosipitali.

Kutokana na idadi kubwa ya wananchi kukumbwa na tatizo hilo la maji, ni dhahiri kuwa wapo wapiga kura wengi wanaoathiriwa na kadhia hiyo. Tunaamini kua vyama na wagombea wa vyama mbalimbali watalifanya suala hili kuwa ajenda kubwa inayohitaji mikakati inayotekelezeka hivyo kutatua kero ya maji nchini.


Hivyo ni wito wetu kwa wanasiasa nchini kuwatua ndoo kichwani wananchi hasa wanawake badala ya kuwatwisha. Tunawaomba wananchi, vyombo vya habari pamoja na wadau wengine watuunge mkono katika kuleta mabadiliko.  

Post a Comment

0 Comments