RAIS wa bendi ya FM Academia ‘Wazee wa
Ngwasuma’, Nyoshi El Saadat, ametamba kwamba pambano lao na African Stars ‘Twanga
Pepeta’ litakalofanyika viunga vya ufukwe wa Escape One Mikocheni Dar es Salaam
Machi 28 mwaka huu, litaandika historia katika tasnia ya muziki wa dansi na
hata kwa bendi hizo mbili nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam
jana, Nyoshi alisema Ngwasuma wako vizuri hivyo wapinzani wao wanapaswa
kujipanga vilivyo.
“Mimi nawambia bendi ya Twanga Pepeta
wajiandae kupambana na sisi kuanzia mavazi hadi kuwajibika jukwaani, kwa sababu
bendi ya FM Academia imesheheni wanamuziki wenye sifa na wanaoujua muziki wa
dansi,” alisema Nyoshi na kuongeza.
Bendi ya Twanga Pepeta na mashabiki
wake, wajitayarishe kuona viuno vikinengua katika kiwango cha hali ya juu
kutoka kwa wanenguaji wa Ngwasuma.
Naye Kiongozi wa Twanga Pepeta, Luizer
Mbutu, alijibu mapigo kwamba, siku hiyo wataanza na Nyoshi kwa kumfundisha
namna ya kuimba katika lugha ya Kiswahili fasaha.
“Twanga tutawaonyesha kazi FM kwamba
sisi tunaujua muziki, hivyo siku hiyo lazima wakae na waamuzi watakuwa
mashabiki wenyewe,” alisema Luizer.
Alisema wana safu iliyokamilika, hivyo
mashabiki watarajie kuona wachezaa shoo ambao wataonyesha umahiri wa hali ya
juu pamoja na sebene la nguvu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Twanga
Pepeta, Asha Baraka, aliongeza kuwa maandalizi ya pambano hilo ambalo wana imani kubwa litakuwa la aina
yake na kuandika historia kwenye muziki wa dansi nchini, yanaendelea vizuri chini
ya udhamini wa Clouds Media Group, ambao ndio waliojitokeza kwa sasa.
0 Comments