Baadhi ya Madaktari kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Mifupa (MOI), Hospitali ya Rufaa Mbeya na Rukwa wakimsikiliza kwa makini Mwenyekiti wa Bodi ya NHIF. |
Na Grace Michael
MAMIA ya wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali katika Mkoa wa Katavi wamekutana na Madaktari bingwa waliokwenda mkoani humo kupitia mpango unaoendeshwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya wa kupeleka madaktari bingwa katika mikoa ya pembezoni.
Timu ya Madaktari hao ilianza kazi rasmi jana ambapo ilifanikiwa kukutana na jumla ya wagonjwa 176 ambao kati yao ni wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) na wananchi wengine ambao hawajajiunga na utaratibu wa bima.
Kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi wa mkoa huo, leo (Jumanne) timu hiyo inatarajia kuhudumia zaidi ya wagonjwa 200 hali inayoonesha uhitaji mkubwa wa huduma za kitaalam katika mikoa ya pembezoni ambayo ina uhaba mkubwa wa wataalam kama hao.
Akifungua zoezi hilo katika Hospitali ya Mpanda, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Balozi Ali Mchumo alitumia mwanya huo kuwahamasisha wananchi mkoani hapo ambao hawajajiunga na NHIF/CHF kuchangamkia fursa hiyo ili wawe na uhakika wa kupata matibabu wakati wowote hata kama hawana fedha.
Pia aliwataka watoa huduma kuendelea na uboreshaji wa huduma za matibabu katika vituo vyao ili kuwavutia wananchi kujiunga na huduma za Mfuko ambazo kwa sasa ni mkombozi wa Watanzania wengi.
“Uongozi wa Mfuko hautachoka kuendelea na jitihada za uboreshaji wa huduma katika sekta ya afya na ndio maana tumeona tuanze huu mpango ili kila Mtanzania bila kujali alipo anufaike na utaalam wa hawa Madaktari bingwa ambao ni wachache kwa nchi yetu,” alisema Balozi Mchumo.
Naye Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Emanuel Humba aliuomba uongozi wa mkoa huo kuendeleza uhusiano na ushirikiano mzuri baina yake na Mfuko ili kuweza kufikia malengo ya kuwaingiza wananchi wengi zaidi katika huduma za Mfuko.
Kwa upande wa wananchi waliofika hospitalini hapo kupata huduma za wataalam hao, waliupongeza Mfuko na kuushukuru kwa jitihada zake ambazo zimekuwa zikionekana wazi muda wote lakini pia kwa kuona umuhimu wa kupeleka huduma hizo katika mikoa hiyo ambayo kwa muda mrefu imekosa huduma hizo.
Madaktari hao watatoa huduma mkoani humo kwa muda wa siku saba na badae kuelekea mkoani Rukwa.
0 Comments