Kikosi cha Taswa Fc.
Kikosi cha Taswa Queens.
*************************************
Na Mwandishi Wetu
TIMU
ya soka ya waandishi wa habari za Michezo nchini (Taswa FC) na timu ya
netboli (Taswa Queens) itaondoka jijini Jumatano alfajiri kwenda Kibiti, mkoa wa Pwni kwa ajili ya mechi maalum ya kirafiki.
Mechi hiyo imepangwa kufanyika kwenye uwanja wa Samora imeandaliwa kwa ajili ya kuanzisha uhusiano wa karibu baina ya waandishi wa habari za michezo na walimu wa wilaya hiyo katika kuendeleza sekta hiyo hapa nchini.
Mwenyekiti
wa Taswa FC, Majuto Omary alisema kuwa mechi ya kwanza siku hiyo
itakuwa kati ya Taswa Queens na kombaini ya walimu iliyopangwa kuanza
saa 9.00 ambapo mechi ya pili itakuwa kati ya Taswa FC na kombaini ya
walimu iliyopangwa kuanza saa 10.00 jioni.
Majuto
alisema kuwa mbali ya kuanzisha uhusiano na kupromoti michezo katika
wilaya hiyo, mechi hizo pia zitakuwa sehemu ya maandalizi ya Taswa FC na
Taswa Queens kwa ajili ya ziara ya kimichezo mkoani Arusha na Tanga
mwezi ujao.
“Maandalizi
ya safari yamekamilika na tunawaomba wachezaji wazingatie muda wa
kufika ili tuweze kuondoka kwa mujibu wa ratiba yetu, lengo ni kuwahi
kufika na kumaliza mapema na kuendelea na ratiba nyingine kwa mujibu wa
wenyeji wetu,” alisema Majuto.
Alisema
kuwa timu zao zote zimejiandaa kwa ushindi katika mechi hizo ambazo
zinatarajiwa kuwa na ushindani mkali kutokana na maandalizi. Taswa FC
haijapoteza hata mechi moja tokea kuanza kwa mwaka huu. Timu zote mbili
zilitoa vipigo kwa timu ya Kiliflora ya Arusha kwa mabao 4-1 kwa upande
wa soka na mabao 28-8 kwa upande wa netiboli.
Mratibu
wa mechi hiyo, mwalimu Paul Nyoni amesema kuwa maandalizi yote
yamekamilika na wanawasubiri kwa hamu waandishi wa habari. Nyoni alisema
kuwa wamewaandalia mapokezi mazuri kwa waandishi na wanaamini mechi
hizo mbili zitakuwa na mvuto na ushindani mkubwa.
0 Comments