Dar es Salaam
Ujumbe maalum kutoka Chama cha Waandishi wa Habari wa Ufalme wa Oman (OJA), uliopo nchini leo Agosti 19, 2026 umefanya mazungumzo na Chama cha wafanyakazi katika vyombo vya habari (JOWUTA) na Serikali na kukubaliana kuandaa kongamano la kimataifa ambalo litahusisha wanahabari wa nchi hizo na sekta nyingine.
Makubaliano hayo yamefikiwa katika ziara ya kikazi yenye lengo la kuimarisha uhusiano wa kitaalamu na kindugu, baina ya Oman na Tanzania, mazungumzo ambayo yamehudhuriwa pia na maarifa wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Idara ya Habari - Maelezo Jijini Dar es Salaam.
Ujumbe huo wa OJA, uliopo nchini kwa mwaliko wa JOWUTA, unaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa OJA, Salem Hamad Al-Jahwari.
Akizungumza katika kikao hicho, Al-Jahwari alieleza kuwa ziara hiyo inalenga kujenga nguzo thabiti za ushirikiano zitakazowezesha kubadilishana uzoefu, kutoa mafunzo ya kitalaamu, na kujengeana uwezo wa kiutendaji baina ya waandishi wa habari wa nchi hizo mbili.
Aidha, alibainisha kuwa ajenda kuu ya ziara hiyo ni kufanya majadiliano na uongozi wa JOWUTA pamoja na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya kongamano la pamoja la waandishi wa habari linalotarajiwa kufanyika hapa nchini baadaye mwaka huu.
Al-Jahwari alifafanua kuwa kongamano hilo, ambalo linayalenga maeneo ya kimkakati kama vile biashara, uwekezaji, utalii na habari ili kuibua fursa za ushirikiano wa kiuchumi, litakuwa la pili kufanyika Barani Afrika baada ya lile lililofanyika nchini Misri.
Kongamano la aina hiyo limewahi kufanyika pia katika nchi za Uingereza, Marekani, China, na Uturuki.
"Oman na Tanzania zina uhusiano wa kihistoria wa kindugu wa zaidi ya miaka 150.
Hivyo, tumeona ni busara kuja Tanzania kufungua milango ya ushirikiano wa moja kwa moja baina ya wanahabari wetu, kwani serikali zetu zina uhusiano wa kihistoria wa muda mrefu," alisema Al-Jahwari
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari-Maelezo Evod Kyando aliipongeza JOWUTA kwa hatua yake ya kupanua wigo wa ushirikiano na taasisi za kimataifa, akisema juhudi hizo zinasaidia kwa kiasi kikubwa kulitangaza taifa kimataifa.
Aliongeza kuwa kongamano hilo linakuja wakati muafaka na litakuwa chachu ya kukuza uchumi kupitia sekta za kipaumbele kama utalii, biashara na uwekezaji, jambo litakalochochea maendeleo ya nchi zote mbili.
Naye Katibu Mkuu wa JOWUTA, Selemani Msuya, alisisitiza kuwa ushirikiano huo mpya kati ya JOWUTA na OJA utaleta tija kubwa kwa wanachama na waandishi wa habari kwa ujumla, hususan katika nyanja za mafunzo ya vitendo na kubadilishana uzoefu wa kiuhariri na kiuchunguzi.
“Sisi JOWUTA tunawashukuru OJA kwa kutambua uwepo wetu na kutushirikisha katika kuandaa kongamano hili la Kimataifa, tutahakikisha tunalitumia kuitangaza sekta ya habari na nchi yetu,” alisema.


0 Comments