BLACK LEOPARDS KUVAANA NA YANGA


 Baadhi ya wachezaji wa timu ya Black Leopards ya Afrika Kusini wakiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam jana. Timu hiyo inashuka dimbani leo kupambana na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa katika mchezo wa kirafiki. 
 Kikosi cha timu ya Black Leopards kikiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kuwasili leo.


DAR ES SALAAM, Tanzania

WAKATI mabingwa wa soka wa Afrika Mashariki na Kati, Yanga kesho watacheza mechi ya kwanza ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya timu ya Black Leopards ya Afrika Kusini, kocha wa Black Leopards ametema cheche na kusema wataibuka na ushindi mkubwa kutokana na uzoefu wao wa mashindano ya Kimataifa.
Mchezo huo umepangwa kuanza saa 10.00 jioni na maandalizi yake yamekwisha kamilika huku waandaaji wakipunguza viingilio ili kuwawezesha mashabiki wengi kufika.
Mratibu wa mechi hiyo, Shafii Dauda wa Prime Time promotion alisema jana kuwa maandalizi yote yamekamilika na wamepunguza kiingilio cha shs 5,000 na shs 7,000 na kuwa cha shs 3,500 ili kuwafanya mashabiki wengi kuona mechi hiyo.
Viingilio vingine ni shs 7,000 kwa viti vya rangi ya machungwa, wakati VIP C ni shs 15,000 , VIP B shs 20,000 na VIP A shs 30,000
Dauda alisema kuwa Black Leopards wamewasili na kutamba kushinda mechi hiyo kutokana na uzoefu waliopata katika mashindano mbali mbali ikiwa pamoja na kombe la Shirikisho.
Kocha wa timu hiyo, Abel Makhubela alisema kuwa wanauzoefu wa siku nyingi na walifanya ziara nchi mbali mbali katika afrika na kuja Tanzania ni moja ya faraja kwao.
“Ziara hii ziara yetu ya kwanza Tanzania, tumefanya ziara nchini Zimbabwe na nchi nyingie, tulipata matokeo mazuri na vile vile tunatarajia kupata matokeo mazuri hapa, nimekuja na wachezaji wangu wote wa kikosa cha kwanza, jumla ya wachezaji ni 23, mashabiki watarajie mchezo mzuri,” alisema Makhubela.
 Alisema kuwa wanaijua Yanga na Simba ni moja ya timu nzuri na maarufu bara la Afrika na hivyo wamejiandaa kwani ni kipimo kizuri cha ligi ya kwao ambayo ipo katikati..

Post a Comment

0 Comments