DAR ES SALAAM, Tanzania
DIWANI wa Kata ya Charambe (CCM), Temeke Abdallah Cahurembo ameanzisha Mfuko wa Mikopo ambao hauna riba kwa ajili ya vikundi vya wajasiriamali katika kata hiyo.
Akizungumza na
vikundi vya akina mama hao, kwenye hafla ya uzinduzi wa Mfuko huo iliyofanyika
jijini Dar es Salaam jana, Chaurembo alisema mfuko huo utasaidia kukuza mitaji
ya kina mama hao ambao ndiyo nguzo ya familia.
Alisema kuwa
ameanzisha mfuko huo mahususi kwa akina mama kutokana na ukweli kwamba wao
ndiyo wanaopambana na matatizo mbalimbali ya familia ikiwemo kusimamia afya na
maendeleo ya watoto.
“Nilikuwa na
uwezo wa kuanzisha mfuko kama huo kwa ajili ya vijana au hata wakina baba
lakini nimeona wakina mama ndiyo wenye majukumu makubwa katika jamii yetu tofauti
na sisi akina baba”alisema.
Aidha,
Chaurembo alikabidhi sh 200,000 kila kikundi kati ya vikundi sita
vilivyojitokeza kwenye hafla hiyo, ambapo aliwaasa vikundi hivyo vilivyopata
mkopo huo, wakazitumie katika malengo waliyokusudia na si vinginevyo.
Alisema huo ni
mkopo, kila kundi kitakachofanikiwa kumaliza mkopo huo kitaweza kupata mwingine
zaidi yaw a awali.
“Fedha zipo
kwa Ofisa Maendeleo wa kata hiyo, ni akina mama wenyewe kujipanga katika
vikundi ili kupatiwa mafunzo ambayo yatawasaidia kuendesha biashara zao kwa
ufanisi bila kubahatisha, hayo ndiyo masharti ya mkopo huu”alijinasibu.
Akizumzia
mkopo huo kwa niaba ya wenzake, mmoja wa wanavikundi hivyo, Zena Said , alisema
watahakikisha wanaitumia vyema fursa hiyo, bila kumuangusha diwani wao kwani
hiyo ni mara ya kwanza kutokea katika kata hiyo kwa diwani kuanzisha mfuko kama
huo, unaowalenga wanawake pekee.
Awali mgeni
rasmi Peter Kirenge ambaye ni Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), alisema
hatua aliyochukuliwa diwani huyo, haifai kubezwa bali inapaswa kuigwa na
viongozi mbalimbali ikiwa wa vyama vya siasa au hata wadau mbalimbali, kwa
kutoa mikopo isiyokuwa na kero kama vile riba kubwa ambayo wakati mwingine
husababisha akina mama hao kushindwa kulipa na kunyang’anywa mali zao.
0 Comments