MECHI ya mchujo ya Kombe la Dunia Kanda ya Afrika kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Gambia (The Scorpions) iliyochezwa Juni 10 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 124,038,000.
Mapato hayo yametokana na washabiki 31,122 waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo kwa viingilio vya sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000, sh. 20,000 na sh. 30,000. Washabiki 25,901 walikata tiketi za sh. 3,000.
Asilimia 18 ya mapato hayo ambayo ni sh. 18,921,050.85 ilikwenda kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) wakati gharama kabla ya mgawo zilikuwa tiketi (sh. 6,555,000), bonasi kwa Taifa Stars (sh. 15,767,542.37), waamuzi (sh. 13,372,000), usafi na ulinzi (sh. 2,350,000), maandalizi ya uwanja- pitch preparation (sh. 400,000), Wachina- Beijing Construction (sh. 2,000,000), umeme (sh. 300,000) na mafuta ya jenereta (sh. 200,000).
Kwa upande wa mgawo asilimia 20 ya gharama za mechi ni sh. 12,834,481, asilimia 10 ya uwanja sh. 6,417,241, asilimia 5 ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) sh. 3,208,620, asilimia 20 ya Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 12,834,481 na asilimia 45 ya TFF (sh. 28,877,583).
30 WAINGIA KOZI YA KUJENGA AFYA YA FIFA
Walimu 18 wa shule za msingi na makocha 12 wa mpira wa miguu wanashiriki kozi ya mpango maalumu wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) kwa ajili ya kujenga afya kupitia mpira wa miguu.
Kozi hiyo ya siku tano inayoitwa FIFA 11 for Health imeanza leo (Juni 11 mwaka huu) kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na itamalizika Juni 15 mwaka huu.
Mafunzo hayo yanaendeshwa na wakufunzi kutoka FIFA ambapo ujumbe katika 11 for Health ni 1. Cheza mpira, 2. heshimu wasichana na wanawake, 3. jikinge na virusi vya Ukimwi (HIV), 4. epuka dawa za kulevya, pombe na sigara, 5. tumia neti zenye viuatilifu, 6. nawa mikono yako, 7. kunywa maji salama, 8. kula chakula chenye mpangilio, 9. pata chanjo, 10. tumia dawa sahihi na 11. cheza mchezo mzuri.
Walimu hao kutoka shule za Mkoa wa Dar es Salaam ni Aloyce Rutta (Montfort, Temeke), David Kazinge (Temeke, Temeke), Rajabu Ased (Mtoni Kijichi, Temeke), Mathew Kambona (Mji Mwema, Temeke), Ruth Mahenge (Chang’ombe, Temeke), Abdul Mikoroti (Nzasa, Temeke), Exuperus Kisaka (Mavurunza, Ilala), Khadija Kambi (Karume, Ilala) na Hamisi Ibrahim (Tusiime, Ilala).
Wengine ni Baltazar Kagimbo (Tabata Jica, Ilala), Isaac Mhanza (Airwing, Ilala), Baraka Baltazar (Muhimbili, Ilala), Job Ndugusa (Upanga, Ilala), Tumaini Hiluka (Buguruni, Ilala), Maua Rashid (Uhuru Wasichana, Ilala), Mussa Kapama (Bunju A, Kinondoni), Raymond Rupia (St. Anne Maria, Kinondoni) na Priscus Shilayo (JK Nyerere, Kinondoni).
Kwa upande wa makocha ni Dismas Haonga, Frank Mwakang’ata, John Sebabili, Michael Bundala, Peter Manyika, Raphael Matola, Renatus Magolanga, Robert Mayunga, Said Pambaleo, Seba Nkoma Titus Michael na Wilfred Kidao.
Programu hiyo inalenga watoto ambapo washiriki watakaofaulu katika kozi hiyo ndiyo baadaye watakuwa wakufunzi kwa ajili ya kuifanya katika maeneo mbalimbali nchini.
FIFA YANOA WAAMUZI WAKE, CHIPUKIZI
Waamuzi 54 wanashiriki kozi ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) iliyoanza leo (Juni 11 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kozi hiyo itakayomalizika Juni 14 mwaka huu inaendeshwa na wakufunzi wawili kutoka FIFA wakisaidiwa na wakufunzi wengine wanne wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF). Wakufunzi wa FIFA ni Carlos Henriques na Mark Mizengo.
Wakufunzi kutoka TFF ni Kapteni mstaafu Stanley Lugenge, Leslie Liunda, Soud Abdi na Riziki Majala. Waamuzi wanaoshiriki ni 14 wa Tanzania wenye beji za FIFA ambao ni Erasmo Jesse, Ferdinand Chacha, Hamis Changwalu, Hamis Maswa, Israel Mujuni, John Kanyenye, Josephat Bulali, Judith Gamba, Mwanahija Makame, Oden Mbaga, Ramadhan Ibada, Saada Tibabimale, Samuel Mpenzu na Sheha Waziri.
Washiriki wengine ni 20 wa daraja la kwanza (class one), kati ya hao watano wanatoka Zanzibar. Lakini vilevile wapo waamuzi chipukizi (watoto) 20 ambao mwaka jana walitumika katika michuano ya Kombe la Uhai na Copa Coca-Cola.
0 Comments