KANISA KATOLIKI LAKEMEA UTOAJI MIMBA

Na Happy Mnale , aliyekuwa Dodoma

KANISA Katoliki  limelitaka shirika la Kutetea Uhai Tanzania (PRO-LIFE TANZANIA) kuwasaidia watu kuona ubaya wa vitendo vya utoaji mimba ikiwemo kuwajenga kiimani,kuwaongoza na kuwaonyesha waliokata tamaa huruma ya Mungu ili wapate msamaha na si kuwa kuwa chombo cha kisiasa au kuwatisha watu.

Akizungumza jana katika misa ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto Asiyezaliwa iliyofanyika katika Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Askofu wa Jimbo Katoliki la Dodoma, Mhashamu Gervas Nyaisonga alisema kuwa shirika hilo likisimama kwa dhati na kuondoa woga kusimamia haki litawezesha taifa kusimama na kuwa na watu bora.

Nyaisonga alisema kuwa mataifa yaliyohalalisha njia hizo waametambua uovu huo wa kudhibiti uzazi kwa njia za vidhibiti mimba na utoaji mimba,pro life isisitize pia kutoa elimu kuhusu kuwajibika katika kuzaa sio kwa utoaji mimba.

“kampeni ya kutokuzaa imeshakomaa ndo sababu nchi nyingi zilizoruhusu jambo hilo zinapata shida hivyo Tanzania hatutakiwi kufika huko ni lazima tulikomboe taifa letu,sisi wote wana prolife Injili ya Yesu inatuhubiria juu ya uhai na kuutunza, sote tuwe walinzi wa uhai,tusimame imara ili tuwe na uzima wan chi,uzima wa taifa”alisema Askofu

Naye Mkurugenzi wa Shirika hilo Emil Hagamu alisema kuwa wanaitumia siku hiyo kama moja ya mikakati ya kulaani vitendo vya utoaji mimba unaofanyika kwa njia za kienyeji au kwa kutumi a wahudumu wa afya.

“Tunaitumia siku hii katika kupinga kutungwa kwa sheria za kutoa mimba tunataka kusema hapana kwa vitendo hivyo,ili kila mmoja aelewe kuwa kutoa mimba ni kuua binadamu aliye dhaifu na asiyejiweza kujitetea ni vitendo vya ukatili na unyama vyenye kumwaga damu”alisema Hagamu

Aidha Hagamu alisema kuwa siku hiyo inataka kuwaambia wale wote wanaopigania kutungwa kwa sheria hiyo kuwa wamepungukiwa kiakili ,wanamtumikia Ibilisi ambaye asili yake ni mwongo na muuaji. Hivyo furaha yao ni kuona mizoga ya binadamu ,maiti ambazo hazipewi heshima ya kushirikishwa maisha ya kikristo kwa njia ya ubatizo na kuzikwa.

Siku hiyo imeadhimishwa kwa lengo kuwaombea wanawake walioua watoto wao kabla ya kuzaliwa,walioshiriki kuangamiza uhai mpya kabla ya kuzaliwa kwa njia ya utoaji mimba,wanaonyanyasa na kuwadhalilisha wanawake,wanaodhalilisha ubaba na umama na mashirika yanayohamasisha kampeni za kutungwa sheria za kutoa mimba,elimu potofu iitwayo afya ya uzazi na jinsia ikiwa ni pamoja na kukumbatia utasa kwa njia ya vidhibiti .

Post a Comment

0 Comments