Wadau wa Jukwaa la Sanaa hasa wasanii wakifuatilia hatma ya muswada huo wa hakimiliki na shiriki ambapo kwa pamoja waliomba ufikishwe bungeni haraka ili kulinda haki zao.
Mkongwe muziki nchini Kassim Mapili akishika makabrasha yaliyosheheni masuala mbalimbali ya hakimiliki na hakishiriki kwa wasanii wakati akichangia mada kwenye Jukwaa la Sanaa. Alitaka muswada huo ufikishwe bungeni mapema iwezekanavyo
Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Jehovaness Aikael (Kushoto) akiwaeleza wadau wa sanaa namna serikali inavyopoteza mapato kwa kuchelewa kuhuisha sheria ya hakimiliki kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila Jumatatu kwenye Ukumbi wa BASATA. Katikati ni Msanii mkongwe John Kitime na Afisa Kutoka COSOTA, Doreen Anthony.
Afisa wa COSOTA, Doreen Anthony (Kulia) akiwaonesha wadau wa Sanaa baadhi ya mapungufu yaliyo kwenye sheria ya sasa ya hakimiliki na shiriki kwenye Jukwaa la Sanaa, BASATA. Kulia kwake ni Bw. John Kitime.
Na Mwandishi Wetu
Wasanii nchini wametoka na azimio la kuhakikisha ifikapo Juni mwaka huu muswada wa mahuisho ya sheria ya hakimiliki na hakishiriki Na.7 ya mwaka 1999 uwe umefikishwa bungeni na kupitishwa rasmi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye Jukwaa la Sanaa linalofanyika kila wiki kwenye Ukumbi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) na baadaye kuja na azimio hilo, wasanii hao walisema kwamba, suala la kuupeleka muswada huo bungeni limekuwa likisuasua pasipo sababu ya msingi huku haki zao zikiendelea kupotea na kuwaacha maskini.
“Tunachotakiwa kufanya kwa sasa kama wadau ni kuusukuma haraka iwezekanavyo muswada huu wa hakimiliki ili ufike bungeni. Sheria iliyopo ina mapungufu na changamoto nyingi ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele mara nyingi” alisema John Kitime ambaye ni msanii wa Bendi kongwe ya Kilimanjaro.
Huku akitaja baadhi ya mapungufu ya sheria iliyopo Kitime alisema kwamba, Asasi ya RULU Art Promoters kwa kushirikiana na Shirika la BEST-AC imefanya utafiti wa kina kuhusu mapungufu yaliyoko kwenye sheria ya sasa ya hakimiliki na kuja na mapendekezo kadhaa lakini hadi sasa ni miaka sita bila hatua kuchukuliwa katika kuihuisha sheria hii.
Kwa upande wake msanii wa muziki wa zouk ambaye kwa sasa amegeukia injili, Stara Thomas alisema kwamba, hakuna nia ya dhati ya kurekebisha sheria hiyo ndiyo maana pamoja na mapendekezo kufikishwa Wizara ya Viwanda na Masoko kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa hakuna kilichofanyika.
“Tuwalilie wabunge wenye uchungu na sanaa yetu wasukume muswada huu, kwa hali ilivyo ya kusuasua unaweza kuchukua muda mrefu kufikishwa bungeni. Ni lazima wasanii tunyanyuke na kudai mahuisho ya sheria hii na kushikamana na wale wanaopigania haki zetu” alisisitiza Stara Thomas.
Akizungumza kuhusu hasara inazopata serikali kwa kusuasua katika kuhuisha sheria hii, Mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Jehovaness Aikael alisema kwamba, utafiti uliofanywa na RULU Art Promoters unaonesha kwamba, sekta ya muziki pekee inaweza kuchangia asilimia moja ya pato la taifa.
“Sekta ya muziki pekee kama ikisimamiwa na sheria safi za hakimiliki na shiriki inaweza kuchangia kwenye pato la taifa kwa zaidi ya asilimia moja. Hapa hatujagusa sanaa nyingine nyingi. Kwa hiyo mtaona ni jinsi gani serikali inapoteza mabilioni kwenye sekta hii” alisisitiza Dkt. Aikael.
Hata hivyo, aliwashauri wasanii kujisajili kwenye Chama cha hakimiliki (COSOTA) na kuwa na umoja thabiti ili kuwa na haki za kumiliki kazi zao na baadaye kuanza kufaidi pale sheria iliyopo itakapohuishwa kwani kwa mujibu wa COSOTA ni wasanii wachache waliojisajili.
0 Comments