KISIWA CHA TEMBONYAMA,MAFIA CHAPATA MWEKEZAJI

Na Mwamvua Mwinyi,Mafia 
Kisiwa cha Tembonyama Kijiji cha Banja Kata ya Kirongwe chenye ukubwa  wa hekari 35 kinatarajiwa kupata mwekezaji atakayeleta mabadiliko ya kiuchumi na mageuzi kwenye utalii, ikiwa ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za Serikali kukuza utalii nchini na kutunza mazingira .

Katika hatua za awali Kamati ndogo ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama Taifa,  imefika kwenye eneo hilo kukagua ili kujiridhisha na hali ya usalama katika kisiwa hicho ,kabla ya kuingia mikataba na mwekezaji.

Kamati hiyo imefika baada ya uamuzi wa pamoja wa wanakijiji cha Banja kupitia Mkutano Mkuu wa kijiji hicho kuomba kutafutiwa mwekezaji ili kijiji kiweze kupata mapato.

Akizungumza na wanakijiji, Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy aliwataka viongozi wa Wilaya, Kijiji pamoja na wananchi kuzingatia hali ya usalama kisiwani hapo na kijiji kwa ujumla kabla na wakati wa kusainisha mkataba na mwekezaji atakayependekezwa pamoja na kujali maslahi ya wananchi.

" Suala la kwanza ni Ulinzi na Usalama, kama hakuna usalama hakuna kitakqchoeleweka" alisisitiza. Walioturithisha nchi hii, waliturithisha ikiwa nzuri na salama, hivyo na sisi tuhakikishe tulichorithishwa tunarithisha na wengine" alisema Meja Jenerali Mkeremy.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia Mhe. Aziza Mangosongo alisisitiza ,ulipaji mzuri wa kodi kwa Halmashauri ili mwekezaji atakayepatikana, aweze kuzingatia makubaliano na vigezo vyote ambavyo vinatakiwa na Wilaya na Taifa kwa ujumla kukwepa upoteaji wa mapato.

Wakazi wa Banja waliishukuru Serikali kwa hatua hiyo na kuahidi kutoa ushirikiano ili kuleta maendeleo katika sekta ya utalii wilayani.

" Kwa niaba ya wazee wa kijiji cha Banja, natoa shukrani nyingi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na tumefurahishwa na wageni wetu, hivyo karubuni sana" alisema Mzee Mohammed Uledi.

Shughuli mbalimbali zinazofanyika katika kisiwa hicho ni uvuvi wa mazao ya bahari mfano uokotaji wa tondo, wananchi kuchuma mboga ya pwani, na uwindaji wa ndege.


Post a Comment

0 Comments