Mchezaji wa timu ya Taifa Stars Shaaban Kado
Na Juma Kasesa
KIPA namba mbili wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na Mtibwa Sugar, Shabani Kado, amefungiwa kucheza mechi tatu na kulimwa faini ya sh. 300,000, baada ya kutiwa hatiani na Kamati ya Mashindano kwakosa la kumtukana matusi ya nguoni mwamuzi wa mchezo wa Ligi Kuu baina ya timu hiyo na Toto Afrika.
Adhabu ya Kado ambaye ameitwa katika kikosi cha timu Taifa kinachojiwinda na mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (CHAN) dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, imethibitishwa jana jijini Dar es Salaam na Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Boniface Wambura, ambapo kipa huyo alimtukana mwamuzi wa mchezo huo na kutolewa nje kwa kadi nyekundu.
Wambura alisema, Kamati ya Mashindano ambayo ilikutana Machi 19 mwaka huu kupitia taarifa mbalimbali za michezo ya Ligi Kuu, pia imepitia ripoti ya ya Kamisaa wa mchezo wa Yanga na Majimaji uliopigwa Februari 5 mwaka huu mjini Songea, na kubaini kuwa wachezaji wa Yanga walivunja viti na mlango wa Mama Lishe na mashabiki wake kufanya vurugu.
Kutokana na tukio hilo Kamati hiyo imelipeleka suala hilo kwa Kamati ya Nidhamu kwa ajili ya kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika, sambamba na tukio la kocha wa Toto Afrika ya Mwanza, Choki Abedi, ambaye alimtukana mwamuzi wa mezani matusi ya nguoni na kutupa chupa ya maji chini katika mchezo baina ya timu hiyo na Simba.
Aidha Wambura alisema, wachezaji wa timu ya Kagera Sugar, Msafiri Devon a David Luhende ambao nao waliwarushia waamuzi chupa za maji katika mchezo dhidi ya Yanga wanatarajiwa kuchukuliwa hatua na Kamati ya Nidhamu kutokana ripoti ya Kamisaa wa mchezo.
Katika hatua nyingine Wambura alisema, mchezo wa Ligi Kuu baina ya Simba na Kagera Sugar, uliopangwa kupigwa Machi 27 jijini, umesogezwa mbele hadi Machi 26 ili kutoa mapumziko ya masaa 24 kwa wachezaji wa Simba ambao walioko katika kikosi cha timu ya Taifa kinachijiwinda na mchezo wa kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Afrika Kati.
0 Comments