WAPENDANAO WAJIVINJARI VALENTINE DAY NGORONGORO


Na Mwandishi wetu, Ngorongoro.

Kama wewe unahisi Penzi lako linalegalega na kuishiwa Pawa hujachelewa, mshawishi mpenzi, mume au mke wako mje Bustani ya Edeni katika hifadhi ya Ngorongoro. Shuhuda za wanyama wakubwa watano, mandhari ya kuvutia yaliyopambwa na sauti za ndege porini pamoja na harufu nzuri ya maua ya bustani ya Edeni yatalipa Nguvu Penzi lako kwa kulinogesha na kuligongelea Msumari.

Mamia wamejitokeza leo tarehe 14/02/2026,  kutembelea Hifadhi ya Ngorongoro kusherehekea Sikukuu ya Wapendanao (Valentine’s Day), wakichagua hifadhi hiyo kama sehemu maalum ya kuonesha mapenzi na kufurahia vivutio vya utalii kwenye kivutio cha utalii namba moja Afrika.
Watalii waliotembelea Ngorongoro  wameshiriki matembezi ya utalii, upigaji picha za kumbukumbu na shughuli mbalimbali zilizowawezesha kufurahia mazingira ya hifadhi kwa namna tofauti na sherehe za mijini. 

Mmoja wa watembezi hao Juma Shemoka na Mpenzi wake Radhia El-had wanaelezaa uzoefu huo umeongeza thamani ya sikukuu hiyo kwa kuunganisha burudani, mapumziko na kujifunza kuhusu uhifadhi wa mazingira na jinsi Wanyamapori wanavyoishi na kuthihirisha thamani ya upendo.

Hivi karibuni mamlaka hiyo ilizindua huduma mpya ya Wedding Tourism, inayowezesha wanandoa na wachumba kufanya harusi, kuvishana pete pamoja na sherehe nyingine za kimahaba ndani ya maeneo ya hifadhi ambapo huduma hiyo inalenga kupanua bidhaa za utalii na kuvutia makundi mapya ya wageni wa ndani na nje ya nchi kufurahia mapenzi ndani ya maeneo tulivu ya hufadhi.
Akizungumza kuhusu mafanikio hayo, Afisa Masoko Mkuu  Ngorongoro, Michael Makombe, alisema mwitikio mkubwa wa wananchi unaonesha kuwa juhudi za kukuza utalii wa ndani zinaendelea kuleta matokeo chanya. 

Karibu Ngorongoro ambapo maajabu saba yanayojumuisha asili ya binadamu, mazalia ya nyumbu, Kasoko ya Ngorongoro, maisha ya watu, wanyamapori, malikale, Jiolojia na vingine vingi vinakutana katika eneo moja.

Post a Comment

0 Comments