Mnenguaji nyota katika tasnia ya muziki wa dansi hapa nchini, mbaye alikuwa akiitumikia bendi ya The African Stars 'Twanga Pepeta' Susan Chubwa almaarufu kwa jina la ‘Queen Suzy’ kesho usiku anatarajiwa kutambulishwa rasmi katika bendi yake ya zamani FM Academia 'Wazee wa Ngwasuma' , utambulisho huo utafanyika katika onyesho lao ambalo litakalofanyika katika ukumbi wa Kijiji Cha Makumbusho.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar es Salaam leo mchana , Queen Suzy amekiri kuwa, amerudi tena kuitumikia bendi ya FM Academia na kuanzia kesho ataonekana katika maonyesho yote ya bendi hiyo.
Mnenguaji huyo ambaye alijiunga na Twanga Desemba mwaka 2009 katika ukumbi wa Club Bilicanas ambapo alitambulishwa na rasmi katika usiku wa Mwafrika unaorindima kila siku ya Jumatano ambako amedumu katika bendi ya Twanga kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoj a.
Aidha mwishoni mwa mwaka jana Suzy na mpenzi wake G7 ambaye pia ni Rapa wa FM Academia walikwenda Umangani na mara baada ya kurudi hajawahi kupanda jukwaani hadi leo mchana zilipopatikana habari za ndani kwamba anarudi FM Academia.
Akielezea sababu ya kurudi tena katika bendi hiyo, Suzy alisema kuwa amefanya hivyo ili aweze kufanya kazi pamoja na mpenzi wake , Aime Chad Mwamba ‘G7’, ikiwa ni katika kuepusha migogoro iliyokuwa ikitoa baina yao .
“Wewe mwenewe ulikuwa unaona jinsi tunavyogombana kila siku , ugomvi hauishi mambo mengi yamesemwa juu yangu hivyo bora tukae pamoja kila mtu awe na imani na mwenzake , pia aliongeza kwa kusema ,itabidi bendi ya Twanga wanisamehe, kwa sababu imenilazimu kufanya hivyo pamoja na kubadilisha upepo katika kazi, sina ubaya nao nawaheshimu sana na Twanga ni nyumbani kwangu na haya ni maisha huenda kesho nikarudi tena , nilishawahi kucheza katika bendi ya Tam Tam wakati wa enzi za Muumini , hivyo nawatakia wabaki kwa amani,” alisema Queen Suzy.
Naye Meneja wa bendi ya FM Academian Kelvin Mkinga alisema, wamempokea Queen Suzy kwa mikono miwili kwani mnenguaji huyo alikwenda kuomba kazi yeye mwenyewe, hivyo kutokana na kutambua mchango wake wakati alipokuwa akifanya kazi Ngwasuma, kabla hajaipa kisogo, uongozi umeamua kumrudisha kundini.
Akizungumza na Mwandishi wa habari hizi jana, Kiongozi mmoja wa bendi ya Twanga alisema, taarifa za kuhama mnenguaji huyo machachari awapo jukwaani zilikuwepo na sasa zimetimia.
4 Comments
Adam Kajonje,Msasani.