VIINGILIO SIMBA YANGA VYATAJWA

kikosi cha timu ya Yanga
Kikosi cha timu ya Simba.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vya mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga iliyopangwa kufanyika Oktoba 16 mwaka huu katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ambapo kiingilio cha chini ni shilingi 5000.
Akitangaza viingilio hivyo jijini Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa (TFF) Sunday Kayuni, alisema, viingilio hivyo vimepangwa kwa kuzingatia hali za Watanzania ili waweze kumudu kuingia uwanjani kushuhudia mechi hiyo inayovuta hisia za mashabiki wengi nchini.
Tayari Simba wameshatua jijini Mwanza kujichimbia kujiandaa na mechi hiyo huku Yanga wakiwa wamepiga kambi yao nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam katika Wilaya ya Bagamoyo.Alisema viingilio hivyo vimepangwa katika madaraja matatu ambapo kiingilio cha juu kitakuwa shilingi 30,000 kwa VIP A, VIP B shilingi 20,000 na mzunguko shilingi 5,000.
Mechi hiyo inachezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, ikiwa ni miaka 26 imepita bila timu hizo kukutana katika uwanja ikihusisha mechi ya Ligi Kuu zaidi ya kukutana katika mashindano mengine.
Wakati huohuo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Leodgar Chilla Tenga, ameondoka nchini jana kuelekea jijini Cairo akiwa na Mkurugenzi wa Ufundi wa (TFF) Sunday Kayuni na Kocha Mkuu wa timu ya Taifa Jan Poulsen kwa ajili ya kwenda kufanya tathimini ya fainali za mashindano ya(AFCON) zilizofanyika nchini Angola.Alisema katika mkutano huo ambao umeandaliwa na Shirikisho la Soka Duniani FIFA kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Afrika CAF, Tenga anatarajiwa kuwasilisha mada kwa wajumbe wa mkutano huo.
Alifafanua kuwa kikao hicho ni cha kawaida kwa CAF kufanya tathimini ya mashindano yake kama ilivyo kwa mashirikisho mengine duniani ikiwemo UEFA.

Post a Comment

0 Comments