Nikiwa ni kiongozi mkuu wa taasisi isiyo ya kiserikali wala kisiasa Ndani na nje ya nchi, Miss Tourism Tanzania Organisation; ambayo malengo yake makuu ni pamoja na kutangaza na kuhamasisha Utalii na Utamaduni wa Tanzania kitaifa na kimataifa, kuhamasisha jamii kupiga vita umasikini kupitia sekta ya Utalii na Utamaduni, kutangaza mianya ya uwekezaji iliyopo Tanzania na kuhuisha uelewa na uthamini wa Utalii na utamaduni miongoni mwa jamii ya Kitanzanzania.
Nikiwa ni sehemu ya watanzania wenye dhima ya kuongoza taasisi hii, ambayo kila mwaka zaidi ya warembo 300 hadi 400 hushiriki mashindano yake ya Miss Utalii Tanzania katika ngazi mbalimbali, huku zaidi ya watu elfu 12, wakihudhuria katika ngazi mbalimbali za mashindano haya,na wengine zaidi ya milioni 11 wakiangalia na kufuatilia kupitia vyombo mbalimbali vya habari; na kujikusanyia zaidi ya wapenzi na wadau zaidi ya milioni 8 ndani na nje ya nchi tangu kuanzishwa kwa mwaka 2004.
Nikiwa ninaamini kabisa kwamba sekta ya Utalii na utamadini ndizo sekta pekee, ambazo zinaweza kutokomeza umasikini na kutoa mchango mkubwa katika pato la taifa na kuinua uchumi wa taifa letu. Kama ambavyo inathibitika kuwa sekta ya Utalii inachangia zaidi ya 12% ya ajira zote Duniani, sekta ya Utalii inachangia zaidi ya 25 ya pato lote la pato la kigeni nchini na inachangia zaidi ya 16% ya pato la taifa kila mwaka.
Kwa ukweli huu, ni dhaihiri kiongozi ambaye tunamuunga mkono na tunayeona anayepaswa kuchaguliwa na wadau wote wa sekta ya Utalii, Utamaduni, Sanaa na Michezo ni Yule ambaye sera zake na za chama chake zinaelezea na kuonyesha nia ya kuinua na kufanikisha sekta hizo.
Baada ya kusikiliza, kufuatilia kwa makini tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu mwaka huu, nikiwa mkereketwa wa Utalii na Utamaduni, nimeridhika na kutiwa matumaini na sera za mgombea na chama cha mapinduzi (CCM) Dr.Jakaya Mrisho Kikwete, juu ya uendelezaji, ukuzaji na uimarishaji wa sekta za Utalii, Michezo na Utamaduni, siyo kwa kipindi kijacho cha miaka mitano tu bali hata katika kipindi chake cha miaka mitano iliyopita.
Katika miaka mitano ya uongozi wa Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete, tumeshudia kwa mara ya kwanza sekta ya Utalii ikichuana na sekta nyingine, na kufikia wakati hata kuipiku sekta ya madini katika kuliingizia taifa pato la fedha za kigeni na kuchangia pato la taifa. Ni katika kipindi cha utawala wake ambapo kwa mara ya kwanza tumeshudia serikali ikijibu kwa vitendo kilio cha watanzania wengi cha kutaka nguvu zaidi itumike katika kutangaza vivutio vyetu vya Utalii kimataifa na kitaifa. Ni katika awamu yake ambapo tumeshudia juhudi za kweli za kuhamasisha Utalii wa Ndani na wakitamaduni zikifanyika tena kwa mafanikio. Ni katika awamu yake ambapo tumeshudia watu mashuhuri na wafanya biashara wakubwa wa kimataifa wakihamasika kuja kutalii nchini kwa mara ya kwanza, wakiwemo mmiliki wa timu ya mpira wa miguu ya Chelsea wanamuziki mashuhuri duniani n.k. Ni katika awamu yake ambapo bei za kuingia watanzania katika vivutio vya Utalii vilipunguzwa, ikiwemo bei za kuingia katika hifadhi za Taifa kuwa shilingi 1500 kwa Mtanzania, ambapo tumeshuhudia pia miundombinu katika maeneo ya vivutio vya Utalii ikiimarishwa kuliko wakati mwingine wowote, ikiwemo ujenzi wa mahoteli na viwanja vya ndege karibu katika kila hifadhi ya taifa. Kwa kuthamini ukuaji wa sekta ya Utalii nchini, ajenda ya amani na utulivu imekuwa ni kipaumbele cha uongozi wake ili kuvutia watalii zaidi, hata katika visiwa vya Zanzibar ambako amani ilikuwa ni msamiati mzito, na kufananishwa na mfupa uliomshinda fisi Dr. Jakaya M. Kikwete ameutafuna na leo hii Zanzibar ni kisiwa cha amani upendo, utulivu na kimbilio la watalii wengi zaidi Duniani. Ni mwana mapinduzi, mzalendo na jemedari wa mstari wa mbele ambaye hakusita na hasiti kuunga mkono na hata kusaidia juhudi za kila Mtanzania katika kukuza, kuhamasisha na kutangaza Utalii bila ya kujali haiba, karibu wala utajiri au umasikini wa mhusika.
Tumchague kwa sababu ni katika awamu yake ambapo Soka, Mitindo, Urembo, Filamu na hata fani ya muziki imepiga hatua na kuijengea nchi na wasanii wa fani husika kitaifa na kimataifa. Machache kati ya mengi ni pamoja na kufanikisha ujio wa Timu za Brazil, Ivory Cost na upatikanaji wa makocha wa kimataifa wa soka na hata netiboli. Pia katika awamu yake tumeshuhudia Tanzania ikipewa heshima ya matukio makubwa ya kulitangaza taifa na Utalii wake kwa kuwa wenyeji wa Mashindano ya Dunia na kimataifa ya Urembo, Mikutano mikubwa ya Kidunia; na viongozi wa nchi kubwa Duniani kuja nchini na wakati mwingine kukutana nao nje ya nchi. Katika awamu yake pia tumeshuhudia idadi ya wanamichezo mbalimbali wakitanzania waking’ara katika medani za kimataifa ambako wanacheza au kufanyia kazi; ikiwemo mcheza mpira wa kikapu Hasheem Thabit anayecheza mpira wa kikapu Marekani.
Katika awamu yake ameonyesha juhudi na kuthamini mchango wa Sanaa mbalimbali hata kufikia kuamua kuwajengea wasanii wa muziki studio ya kisasa. Lakini ni katika awamu yake ambapo washiriki wa mashindano ya urembo katika mashindano mbalimbali ya Dunia na kimataifa wameweza kutwaa mataji mbalimbali ya Dunia na kimataifa. Hapa yeye binafsi kwa kuthamini mchango wa Sanaa, michezo na Burudani aliweza kuwaalika wachezaji wa Michezo mbalimbali, washiriki na washindi mbalimbali wa Sanaa ya urembo, mpira, ngoma na muziki na kuwapongeza.
Miss Tourism Organisation inamuunga mkono, itamchagua itampigania na inashauri watanzania wote tumchague, ili Tanzania izidi kung’ara kitaifa na kimataifa katika medani za Michezo, Utalii, Sanaa, Utamduni na Amani.
Mungu Ibariki Tanzania, Mbariki Dr. Jakaya M. Kikwete, Ibariki Miss Utalii Tanzania na wabariki watanzania na wapiga kura wote tumchague DR. Jakaya M. Kikwete atukamilishie programu yake ya miaka 10 kwa Kasi Zaidi, Nguvu Zaidi na Ari Zaidi.
Tuepukane na wanaotishia amani ya nchi, wanaohubiri visasi, chuki na hata visasi vya mifupa, kwani Tanzania yetu ni ya maelewano, upendo, umoja na mshikamano tangu uhuru na hata milele. Tuwe makini sio kila asemaye bwana bwana atatulindia amani na utulivu wetu, na hao tutawatambua hata kwa maneno yao na kauli zao za jazba, uchochezi, na kupakana matope kusiko na tija. Dalili ya mvua ni mawingu. Zimwi likujualo halikuli likakwisha.
Asante,
Gideon Erasto Chipunghelo
Rais/Afisa Mtendaji Mkuu
Miss Utalii Tanzania
0 Comments