TFF watangaza viingilio kati ya Taifa Stars &Morocco

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanika hadharani viingilio vya mechi ya kimataifa kusaka tiketi ya kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika baina ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ na Morocco ambapo kiingilio cha juu ni shilingi 30,000.Akizungumza na Waandishi wa leo jijini Dar es Salaam, Ofisa Habari wa (TFF) Florian Kaijage, alisema, katika viingilio hivyo wamezingatia kilio cha Watanzania wengi kutaka visiwe vya bei ya juu ili waweze kwenda kuishangilia timu yao.Alisema kwa kuzingatia kilio hicho mashabiki watakaokaa jukwaa la rangi ya kijani watalipa shilingi 5,000, kikiwa ndiyo kiingilio cha bei rahisi, viti vya bluu 7,000, rangi ya chungwa nyuma ya jukwaa kuu 10,000, VIP C 15,000, VIP B 20,000 na VIP A 30,000.Kaijage alisema tiketi za mechi hiyo inayotarajiwa kupigwa Oktoba 9 mwaka huu katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, zitaanza kuuzwa kesho katika vituo mbalimbali kuanzia saa 4;30 asubuhi.Kwa upande Rais wa (TFF) Leodger Chila Tenga, alisema utaratibu waliouzindua juzi wa kampeni ya kuishangilia timu ya Taifa, utawasaidia wachezaji kujiamini kushinda katika mechi hiyo muhimu ambayo inayotarajiwa kuwa na ushindani wa aina yake.Alisema kujiamini na kiwango kilichoonyeshwa na timu hiyo katika katika mechi ya awali dhidi ya waarabu wengine Algeria ambapo Stars ilifanikiwa kuwalazimisha sare ya bila kufungana, inampa kiburi cha matumaini kuwa timu hiyo itaweza kushinda mchezo huo na kujiweka katika mazingira ya kufuzu fainali hizo zinazotarajiwa kuchezwa nchini Gabon Equatorial Guinea 2012.“Kwa kiwango walichonacho Stars naamini vijana wetu wanaweza kushinda mechi hiyo, kilichobakia kwao ni kuzingatia mafunzo ya benchi la ufundi na kuwa makini muda wote wa dakika 90 za mchezo wasije wakafanya makosa,”alisema Tenga.Aliwataka mashabiki wa soka wadau wa mchezo huo kujitokeza kwa wingi kuishangilia timu hiyo iweze kushinda hasa ukizingatia TFF imesikiliza kilio chao kwa kuweka viingilio vya bei rahisi.Katika hatua nyingine Tenga amekiagiza chama cha Waandishi wa Habari za Michezo TASWA kukutana na Sekretarieti ya Shirikisho hilo kwa ajili ya kuweka utaratibu wa waandishi wa habari za michezo kuingia uwanjani.Alisema katika siku za hivi karibuni kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa waandishi hao kukosa fursa ya kuingia uwanjani kutokana na sababu mbalimbali hivyo ni vyema TASWA ikakutana na sekretariti hiyo kwa ajili ya kuondoa malalamiko.Tunataka tuweke utaratibu wa waandishi kutumia tiketi au vitambulisho kama wanavyofanya nchi za wenzetu, kwani hatuwezi kurusu watu zaidi ya mia moja kuingia uwanjani kwa kutumia vitambulisho,”alisema Tenga.

Post a Comment

0 Comments