MICHEZO NA BURUDANI WATAKA UCHAGUZI WA AMANI

Na Method Millanzi, Mkuranga

Wanamichezo na wadau wa burudani wilayani hapa, wamewaomba wenzao na wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Jumapili Oktoba 31 huku wakiweka mbele amani na utulivu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wilayani hapa juzi, wadau hao walisema kuwa, baada ya mikikimikiki ya kampeni, sasa ni haki yao ya kidemokrasia kujitokeza mapema vituoni ili kuwachagua viongozi bora watakaolisukuma gurudumu la maendeleo.
“Wanamichezo na wasanii, muwe mstari wa mbele kupiga kura Oktoba 31 ili kuweza kuchagua viongozi bora kwa manufaa ya sekta yetu na taifa kwa ujumla,” alisema Alloyce Mnana.
Aidha, Mnana alitoa wito kwa wazee, viongozi wa dini na wanasiasa kuungana nao na kutumia muda uliobaki kuhamasishana amani na utulivu kwenye zoezi hilo nyeti la kuwachagua viongozi wa taifa.
Naye Kachenje wa Vikindu, aliwataka viongozi ambao kura zao hazitatosha, kujenga utamaduni wa kuyakubali matokeo na kuwaelekeza wafuasi wao kudumisha amani iliyoasisiwa na hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Post a Comment

0 Comments