BI KIDUDE NA OFFSIDE TRICK KUPAMBA UZINDUZI WA 5 STARS MODERN TAARAB

PICHANI NI KIKONGWE FATMA BINT BARAKA almaarufu kwa jina la Bi Kidude

Msanii kikongwe nchini wa muziki wa taarab nchini Fatuma Baraka almaarufu kwa jina la Bi Kidude akiwa na kundi la Offside Trick 'Wanaotamba na kibao cha Ahmada' watashiriki uzinduzi wa albamu mbili wa kundi la taarab la Five Stars Modern Taarab utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari, rais wa kundi hilo, Ally Juma 'Ally J', alisema wasanii hao wamekubali kuwasindikiza katika uzinduzi wao.

“Hawa wamekubali kutusindikiza, wameahidi kutoa burudani nzuri zikiwemo nyimbo zao mpya,” alisema.

Ally J, alizitaja albamu hizo mbili ni Shukrani kwa mpenzi na Ndio Basi Tena ambazo tayari zilianza kusikika katika kumbi mbalimbali wanazofanya maonesho.

Alizitaja nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ni Shukrani kwa mpenzi uliobeba jina albamu, Dunia, Bibi wizi mtupu, Hanishushi, Basi tena Ukisema cha nini, Ndio Basi Tena, La uchungu na Paka Mapepe.

“Tumejiandaa vizuri kwa uzinduzi wa albamu zetu mbili, tuna imani zitapendwa na mashabiki wa muziki huu kama ilivyokuwa albamu yetu ya kwanza ya ‘Riziki Mwanzo wa Chuki’,” alisema.

Alisema katika uzinduzi huo kiingilio kimepangwa kuwa sh. 7,000, ili mashabiki wa muziki wa taarab waweze kushuhudia kwa wingi na kila mmoja atapata kanda ya kaseti moja bure.

Wasanii watakaoonekana jukwaani wakiimba nyimbo hizo ni Jokha Kassim, Issa Kamongo, Issa Kijoti, Hussein Mohamed 'Hammer Q', Mariam Hamis, Zena Mohamed, Mwamvita Shaibu na Husna Mapande.

Uzinduzi huo umedhaminiwa na kampuni ya Bussines Times Limited (BTL) inayochapisha magazeti ya Dar Leo na Majira.

Post a Comment

0 Comments