Mzee Kingunge aibuka, ashangaa wanamuandama Lowassa, ashtushwa Mawaziri kuitwa Mizigo


Mzee Kingunge Ngombale Mwiru akisisitiza jambo alipokuwa akizungumza na MICHARAZO nyumbani kwake jana jijini Dar es salaam.
WAKATI makada wa CCM wakilumbana juu ya kitendo cha Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kujitokeza hadharani na kuonyesha nia ya kuwania Urais Uchaguzi wa 2015, mwanasiasa mkongwe Kingunge Ngombare Mwiru ameibuka na kusema haoni tatizo na kilichofanya na Mbunge huyo wa Monduli.
Aidha Kingunge amesema amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na baadhi ya viongozi wakuu wa CCM kuwaumbua na kuwadhalilisha baadhi ya mawaziri wa serikali yao kwa kuwaita 'mizigo', akidai kama walikuwa na makosa katika utendaji wao walipaswa kukosolewa ndani ya vikao vya ndani vya chama chao badala ya kuvuana nguo hadharani na kukiaibisha chama.
Kwa wiki sasa kumekuwa na malumbano baina ya wanaCCM wakimnyooshea kidole Lowassa anayedaiwa kuanza kufanya kampeni zinazohisiwa ni harakati zake za kuwania urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwakani.
Miongoni mwa waliomshambulia Lowassa ni Katibu wa Idara ya Uhamasishaji na Chipukizi-UVCCM, Paul Makonda na Waziri Mkuu Mstaafu, John Malecela.
Viongozi hao wameonyeshwa kukerwa na kitendo kinachofanywa na Lowassa kwa kudai anausaka urais kwa kutumia fedha na kutaka chama kimdhibiti, huku Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula naye akigusia suala hilo na kuwaonya wanachama walioanza kampeni kabla ya wakati.
Hata hivyo Kingunge, akizungumza na MICHARAZO jana nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, alisema haoni tatizo kwa Lowassa na hata mwanachama yeyote ndani ya CCM kujitokeza na kuonyesha dhamira ya kutaka uongozi mapema.
Kingunge alisema kujitokeza mapema kwa mtu mwingine yeyote mwenye dhamira ya kutaka uongozi ni jambo litakalowasaidia wananchi kuwafahamu, kuwajadili na kuwapima kwa kina kuona kama wanafaa kuongoza au la.
Alisema  haoni sababu ya kuibuka malumbano baina ya wanaCCM au kusakamwa kwa Lowassa kwa kitendo chake akidai wengine wanaotaka kufanya hivyo wafanye ili kutoa nafasi kwa wanachama wenzao na wananchi kwa ujumla kuwafahamu na kuwajadili ili ukifika wa uchaguzi wajue la kufanya dhidi yao.
"Sipendi kuingia kwenye malumbano na wanachama wenzangu kwa sababu najua mwishowe watu tunaweza kuvuana nguo, ila kwa mtazamo wangu sioni kama ni kosa kwa wanachama na raia yeyote mwenye nia ya kutaka uongozi kujitokeza na kujionyesha mapema," alisema.
"Kujitokeza kwao mapema kutawafanya wananchi wawaone, wawafahamu, pia wawapime na kuwajadili kwa kina kama wanafaa kubeba majukumu ya uongozi au la, pia sidhani kama ni Lowassa pekee aliyefanya hivyo, vipi asakamwe yeye tu! Siyo dhambi watu wenye nia iwe katika ubunge, udiwani, uenyekiti wa serikali za mitaa na hata urais kuwangong'oneza rafiki na ndugu zao juu ya dhamira yao. Bora hao kuliko wanaofanya mambo yao kwa usiri," alisema.
Mwanasiasa huyo aliyewahi kwa waziri katika serikali za awamu zote nne nchini tangu enzi za Mwalimu Nyerere, alisema tangu enzi za TANU mpaka kuzaliwa kwa CCM upo msisitizo unaosema raia wote wana haki mbili kuu ya kikatiba ya kuchagua na kuchaguliwa, ingawa hawalazimishwi.
"Hakuna anayelazimishwa kuchagua au kuchaguliwa kwa maana ya kuwania uongozi, hivyo kujitokeza kwa wanasiasa na watu wengine kuonyesha nia yao yakutaka uongozi hawafanyi dhambi, hivyo sidhani kuna haja ya suala hili kuwa mjadala mkubwa wakati kuna mambo ya msingi ambayo CCM inapaswa kuyazungumza na kuyajadili kwa kina kwa manufaa ya wananchi," alisema.
Juu ya kitendo cha viongozi wakuu wa Sekretarieti ya CCM kufanya ziara mikoani kisha kutangaza majukwaani majina ya mawaziri walioitwa mizigo, Kingunge kwanza alipongeza ziara hiyo akidai itasaidia kukijenga na kuinua uhai wa CCM, lakini alidai hakubaliani na kilichofanywa na viongozi wao kuwavua nguo watendaji hao wa serikali yao.
Alihoji ina maana viongozi wa CCM hawajui mipaka ya uongozi iliyopo baina yao na serikali iliyopatikana kwa ridhaa ya wananchi.
"Zipo taratibu za kukosoana ndani ya chama, mawaziri ni wabunge, wanaCCM kama wamefanya makosa ilipaswa waitwe na kukosolewa katika vikao vya ndani ya chama badala ya kuwavua nguo hadharani kwa kisingizio wananachi ndiyo wanaowalalamikia. Haya hatukuwatuma," alisema.
alisema yapo mambo ya msingi viongozi wa CCM wanapaswa kuyazungumza na kuyajadili mbele ya wananchi ikiwemo mikakati ya kuwaletea maendeleo ili wafurahie uhuru, pia akidai kwa miaka mingi tangu enzi za TANU, CCM kilifahamika kuwa ni chama cha wanyonge, lakini kwa sasa hilo halipo na kuhoji viongozi hao wanapaswa kuliangalia hilo na kukirejesha chama katika mstari.
"Kama wameshindwa kazi ni vyema wakawapisha wengine wakiongoze, kuliko kukiyumbisha chama na kukifanya kipoteze mvuto mbele ya wananchi kwa kujadili mambo yasiyo na maana kwa wananchi hata kama wanapigiwa makofi, CCM ina sera na taratibu zake za kukosoana kupitia vikaoni, siyo kilichofanywa na viongozi wetu," alisema.
Alisema viongozi wa CCM kwa sasa ni kama wanaoanzisha vita baina yao na watendaji wa serikali kitu ambacho siyo tu kinaonyesha chama chao kuyumba, pia kinaonyesha namna gani wanavyofanya kazi ya kuwasaidia wapinzani badala ya kujijenga na kusaidia serikali yao ili waje kushinda katika chaguzi zijazo.
Kingunge alihoji viongozi waliowaita wanachama wenzao 'mizigo' ndani ya serikali  inayotokana na CCM wanatazamanaje na mawaziri hao kuliorejeshwa.
"Sidhani kama ni jambo zuri, watu waheshimu mipaka ya madaraka yao, wajikite katika kukijenga chama na serikali kwa ujumla badala ya vitu visivyo na tija kwa wananchi iliwayowapa ridhaa ya kuongoza," alisema Kingunge.

Post a Comment

0 Comments