TUNAENDELEA KUBORESHA HUDUMA ZETU KIDIJITALI KUONGEZA UFANISI KWA WAGENI-NCAA

Uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya eneo la Ngorongoro (NCAA) umeeleza kuwa, umedhamiria  kuendelea kuboresha utoaji huduma kwa watalii kwa njia za kisasa kupitia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano ili kuongeza ufanisi na kasi ya utendaji kazi na ukusanyaji wa mapato.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa uhifadhi anayesimamia huduma za Utalii na Masoko Mariam Kobelo ameeleza kuwa lengo la kufanya kazi kidigitali ni kuhakikisha kuwa watoa huduma katika sekta ya utalii wanatumia muda mfupi kuingia na kutoka ndani ya hifadhi pamoja na kuhakikisha maduhuli ya serikali yanakusanywa kikamilifu na kuimarisha usalama wa hifadhi na rasilimali zilizopo.

“Siku mbili zilizopita tumekuwa na changamoto ndogo ndogo  katika lango kuu la Ladoure ,tunaendelea  kuzitatua  kwa ushirikiano mkubwa na wadau wetu”,amesema bi.Kobelo.

Amewashukuru waongoza watalii  wote  na wadau katika sekta hiyo kwa kuonesha ushirikiano wa kutosha katika kufanikisha maboresho hayo.

Ameongeza kuwa mteja yeyote atakayekutana na changamoto za kiutendaji katika kipindi hiki ni vema akawasiliana na maafisa wa mamlaka hiyo ambao wapo katika lango hilo na maeneo mengine na watasaidiwa ili waweze kuendelea na safari zao kwa muda kama walivyopanga.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro katika mwelekeo wa utendaji wake mpya imedhamiria kuimarisha shughuli zake za kutoa huduma bora kwa watalii katika viwango vya kimataifa na kuendelea kuimarisha dawati la huduma na ukarimu kwa wateja.

Post a Comment

0 Comments